Header Ads Widget

WANANCHI WALALAMIKIA POLISI,JWTZ KUKUSANYA USHURU WA MAZAO BILA RISITI

Mbunge wa jimbo la Buhigwe wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma  Felix Kavejuru (kulia) akizungumza katika mkutano wa hadhara wa wananchi kwenye kijiji cha Kilelema wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma katika mpaka wa Tanzania na Burundi.

Diwani wa kata ya Kilelema wilaya ya Buhigwe Hassan Nkatura (kulia) akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa mbunge wa jimbo la Buhigwe uliofanyika kwenye kijiji cha Kilelema mpakani mwa Tanzania na Burundi.

(Picha zote na Fadhili Abdallah)


XXXXXXXXXXXXX

                    Na Fadhili Abdallah,Kigoma                      

WANANCHI wa kijiji ca Kilelema wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma kilichopo mpakani na nchi  ya Burundi wamelalamikia watendaji wa majeshi ya ulinzi na usalama wanaolinda mpaka huo kukusanya ushuru wa mazao bila kufuata taratibu huku wakishindwa kutoa stakabadhi.

Malalamiko hayo yametolewa mbele ya mbunge wa jimbo la Buhigwe, Felix Kavejuru aliyefanya ziara kijijini hapo kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara.

Mmoja wa wananchi hao Samwel Humbiye akizungumza mbele ya mbunge huyo alisema kuwa wanashangazwa na vitendo vya polisi na jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) kukusanya ushuru wa mazao kwa wananchi wanaoenda kwenye masoko ya ujirani mwema nchini Burundi lakini hawatoi risiti hata inapodaiwa.

Alisema kuwa hata wanapodai risiti kutoka kwa watendaji hao wa vyombo vya ulinzi na usalama wanapata vitisho tofauti na mawakala wakukusanya ushuru wa halmashauri ya wilaya Buhigwe ambao wamekuwa wakikusanya ushuru na kutoa risiti kwa kutumia mashine (POS).

Naye Diwani wa kata ya Kilelema, Hassan Nkatura akizungumza kwenye mkutano huo alisema kuwa upo ushahidi wa watendaji wa kikosi cha jeshi la wananchi wanaolinda eneo hilo la mpaka, polisi na wale wa uhamiaji kukusanya fedha kwa wananchi wanaosafirisha mazao kwenda kwenye masoko ya ujirani mwema nchini Burundi lakini hawatoi risiti.

Diwani huyo alisema kuwa wakati watendaji hao wa vyombo vya ulinzi na usalama wakikusanya fedha bila kufuata utaratibu wamekuwa wakitoa vitisho pia kwa wananchi ambao watakuwa wanagoma kutoa fedha hizo kuanzia 5000 hadi 50,000 kwa mtu mmoja.

“Wakati Polisi na jeshi wanafanya hivyo  wapo watendaji wa halmashauri mawakala wa kukusanya ushuru wa mazao ambao wanakusanya fedha na kutoa risiti kwa kutumia mashine za kidijitali kama ulivyo utaratibu hivyo tunashangazwa  wapi fedha hizo za watendaji hao wa vyombo vya ulinzi na usalama zinapelekwa,”Alisema Hassan Nkatura  Diwani kata ya Kilelema.

Akizungumzia malalamiko hayo Mbunge wa jimbo la Buhigwe, Felix Kavejuru amekemea vitendo vya askari hao kukusanya ushuru bila kufuata taratibu na kuwataka kuacha mara moja kufanya hivyo kama utaratibu huo hauzingatii miongozi ya serikali.

 Pamoja na hilo Mbunge huyo alisema kuwa atalichukua jambo hilo na kulipeleka kwa Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Buhigwe ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na kuwabaini wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS