Header Ads Widget

SERIKALI YAANZISHA MIFUMO YA UTENDAJI KAZI MKATABA WA HUDUMA KWA MTEJA

 


Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma


SERIKALI imekuwa ikiweka nguvu nyingi katika kuhakikisha mwananchi anapata huduma bora na kwa wakati na hasa kwa kufanya usimamizi wa viwango vya utendaji kazi Serikalini ili kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa Umma. 


Hivyo kutokana na hayo yote Serikali imeanzisha utaratibu wa kutumia mifumo ya Utendaji kazi ambapo moja ya Mifumo hiyo ni Mkataba wa Huduma kwa Mteja. 


 Akiongea na waandishi wa Habari leo January 31 2023  jijini Dodoma Waziri wa Nchi  Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama wakati akitoa taarifa juu ya utekelezaji wa Mkataba wa huduma kwa mteja katika Taasisi za umma amesema Mkataba wa Huduma kwa Mteja ni ahadi ya kimaandishi kati ya Taasisi ya Umma na wateja wake (Wananchi), 


Amesema Mkataba huo utamuwezesha Mwananchi kufahamu huduma zinazotolewa na Taasisi ya Umma, Viwango vya utoaji wa huduma, Wajibu wa Taasisi kwa mpokea huduma, Wajibu na haki ya mteja au mpokea huduma, Njia zitakazomuwezesha mteja kupokea na kutoa mrejesho wa huduma  zilizotolewa na njia za Mawasiliano na taasisi. 


"Kwa ujumla mkataba wa huduma kwa mteja ni nyenzo ambayo  hutayarishwa kwa ushirikiano na majadiliano kati ya watoa huduma na wadau mbalimbali,"


Na kuongeza Kusema"Kwa mantiki hiyo, ili mtumishi aweze kwenda na kasi ya uwajibikaji atapaswa kuzingatia viwango vilivyowekwa katika huduma anayotoa na kutambua kuwa ni haki ya mteja kupata huduma hiyo kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo katika Mkataba wa Huduma kwa Mteja," Amesema Mhagama

 

Amesema Serikali kupitia  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilishatoa Mwongozo wa  kuziwezesha Taasisi za Umma kuandaa, kuhuisha na kutekeleza Mkataba wa Huduma kwa Mteja. 


"Ofisi hii imekuwa ikitoa utaalaam wa uwezeshaji wa kuandaa mikataba hiyo kutokana na mahitaji ya taasisi kwa ubora na viwango vinavyotakiwa,"


Na kuongeza"  Ofisi hii inalo jukumu la kufanya ukaguzi wa utekelezaji wa Mikataba ili kubaini kama Taasisi za Umma zinatekeleza yaliyomo katika Mikataba yao kwa viwango vilivyokubalika," Amesema Mhagama 

 

Aidha Amesema utekelezaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita  ya kuimarisha utamaduni wa Watumishi wa Umma nchini wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa hiari na bila shuruti na  kuimarisha nidhamu na uwajibikaji katika Utumishi wa Umma, kama Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan alivyoahidi wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Aprili, 2021.

 

Amesema Pamoja na hatua mbalimbali za usimamizi, ukaguzi na ufuatiliaji zinazoendelea kufanyika, Ofisi yangu imebaini maeneo ambayo yanahitaji kutiliwa mkazo katika utekelezaji wa uwepo wa Mikataba ya Huduma kwa Mteja kwenye Taasisi za Umma, maeneo hayo ni kama yafuatayo


Ameeleza Ofisi  imebaini bado kuna baadhi ya Taasisi za Umma hazina Mkataba wa Huduma kwa Mteja, na zile ambazo zina mikataba, Mikataba yake imeshapitwa na wakati au kuandaliwa bila kuzingatia Mwongozo wa Serikali wa kuandaa Mikataba.


Hata hivyo amesema taasisi kwa kutozingatia mwongozo wa uandaaji wa Mikataba ya huduma kwa 

mteja imepelekea taasisi kuwa na mikataba isiyokidhi viwango vya huduma vinavyotakiwa kutolewa, na hii ni kutokana na kukosekana kwa utayari wa Viongozi wa Taasisi za Umma kubadilisha mitizamo ya kiutendaji, kukubali mabadiliko na kuendelea kufanya kazi kwa mazoea kwenye Taasisi zao.

 

Ofisi imebaini baadhi ya Taasisi za Umma hazifanyi  ufuatiliaji wa utekelezaji wa mkataba na kuandaa taarifa na kuiwasilisha kwenye Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora hali inayosababisha Taasisi hizo kuendelea kufanya kazi kwa mazoea bila matokeo tarajiwa.


Amesema ofisi imebaini baadhi ya Taasisi kuandaa/kuhuisha mikataba ya Huduma kwa Mteja bila kushirikisha Wataalam husika na kupata idhini ya matumizi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

 

"Ili kufikia azma ya Serikali tuliyojiwekea, ya kuhakikisha Taasisi zote za Umma ya kuwa na huduma bora zinazotolewa kwa Wananchi wote wa Tanzania na wageni, kupitia Mikataba ya Huduma kwa Mteja Kupitia kikao hiki ninazielekeza Taasisi zote za Umma  (Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma ) kufanya yafuatayo,"


Ameelekeza Kuandaa/kuhuisha Mikataba ya Huduma kwa Mteja ya Taasisi. 


Kuwasilisha katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mikataba iliyoandaliwa au kuhuishwa kwa ajili ya kupata idhini ya matumizi.


Kila Taasisi ya Umma ihakikishe inatangaza Mikataba yake ya Huduma kwa Mteja ili kujenga uelewa kwa wateja wake kuhusu huduma na viwango vya huduma vinavyotolewa na Taasisi


Na pia Kuendelea kufanya ufuatiliaji na tathmini ya viwango vya utoaji huduma vilivyokubalika katika Mikataba, sambamba na kufanya Maboresho stahiki ya Michakato ya Utoaji huduma za Taasisi.


Ili kuhakikisha maelekezo haya ya Serikali yanatekelezwa na wananchi wanahabarishwa viwango vya utoaji wa huduma ndani ya Serikali kupitia Taasisi za Umma, Mikataba itakayowasilishwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kukidhi viwango itazinduliwa kwa pamoja katika  uzinduzi  utakaofanyika katika awamu mbili (2) kama ifuatavyo.


Uzinduzi wa Awamu ya Kwanza  utahusisha Wizara, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, utafanyika  tarehe 28 Februari 2023;


Uzinduzi wa Awamu ya Pili utahusisha Wakala za Serikali, Idara zinazojitegemea na Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali utafanyika tarehe 28 Aprili 2023. 


Taasisi zilizopo katika makundi hayo zinatakiwa kuwasilisha nakala za Mikataba hiyo  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wiki mbili kabla ya tarehe ya uzinduzi. 


"Naomba nisisitize kila mwajiri kuzingatia maelekezo haya ya Serikali," Amesema Mhagama.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS