NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
WANANCHI wa kata za milimani katika Jimbo la Moshi vijijini mkoani wanatarajia kunufaika na Kilimo baada ya Mbunge wa Jimbo hilo, Prof Patrick Ndakidemi kutoa fedha Milioni 74 kwa ajili ya ukarabati wa mifereji ya asili.
Akizungumza katika Kikao cha kawaida cha kamati ya maendeleo mfuko wa Jimbo leo, Mbunge huyo aliishukuru Serikali ya awamu ya sita kumpatia fedha 74,081,500 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika Jimbo la Moshi vijijini ikiwa ni fedha za mfuko wa Jimbo.
Alisema kuwa, kupitia fedha hizo wamekubalia na wajumbe zitumike katika kukarabati wa mifereji ya asili ili kuhakikisha kuwa wananchi ambao shughuli zao kubwa ni Kilimo wanapata maji ya uhakika na kujinufaisha kupitia Kilimo hicho.
"Fedha hizi zimekuja kwa wakati sahihi ambapo kila kata itajipatia saruji mifuko 210 pamoja na milioni moja ambapo mgawanyo utakuwa Milioni 4.5 kwa kila kata kwa ajili ya kununua mchanga ili kukarabati mifereji yote ya asili kwani tunauhakika maji yakiwafikia wakulima watajikwamua vizuri kiuchumi" alisema Prof. Ndakidemi.
Alisema katika kata za Arusha chini ambapo wao hawana mifereji ya asili fedha zake zitaelekezwa katika ujenzi wa ofisi ya kijiji cha Chemchem huku kata ya Mabogini fedha zake zitaelekezwa katika zahanati ya Mvuleni.
Mbunge huyo alisema kuwa, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Jimbo hilo lilipokea Milioni 49,767,000 katika mfuko wa Mbunge lakini kutokana na Sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka jana imepelekea ongezeko la fedha hiyo kufikia 74,081,500 na kuwaomba watendaji kusimamia vyema fedha hizo ziweze kutumika kama zilivyokusudiwa na kuleta matokeo chanya.
Naye Diwani wa kata ya Uru mashariki, Samweli Materu aliishukuru Serikali kwa kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo kwa kuongeza fedha za maendeleo ambapo imetokana na matokeo ya Sensa ya watu na makazi na kuwataka Madiwani wa kata kuhakikisha wanasimamia fedha hizo.
Mwisho...
0 Comments