KATA ya Picha ya Ndege Wilayani Kibaha imekamilisha ujenzi wa vyumba tisa vya madarasa kwenye Sekondari ya Kata na kutumia kiasi cha shilingi milioni 180 zilizotolewa na serikali maarufu kama kapu la Mama Samia hivyo wanafunzi wote 350 waliopangiwa kuingia kidato cha kwanza shuleni hapo kuwa na uhakika wa madarasa.
Akizungumza na waandishi wa habari Diwani wa kata ya Picha ya Ndege Karim Mtambo alisema kuwa shule hiyo kwa sasa kwa upande wa madarasa itakuwa imekamilika.
Mtambo alisema kuwa wanamshukuru Rais kwa kuwapatia fedha hizo ambazo zimejenga idadi kubwa ya madarasa hasa ikizingatiwa shule hiyo bado ni changa.
"Jitihada za serikali zimeonekana kwani mwaka jana tulipata fedha za COVID 19 kiasi cha shilingi milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa nane na sasa tumepata fedha hizo za Mama Samia zimejenga madarasa tisa,"alisema Mtambo.
Aidha alisema kuwa kwa upande wa madarasa hayo mapya yatakayoanza kutumika wiki ijayo yatahitaji kuongezewa viti na meza ili wanafunzi wasome vizuri.
Mwisho.
0 Comments