Kilimanjaro
Serikali imepongezwa kwa kufanikisha kutoa shilingi Bilioni 142 zilizokamilisha uwekezaji wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro ambacho kinachochea uzalishaji ajira na ukuaji uchumi.
Hayo yamejili wakati Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea kukagua mradi wa kimkakati wa uzalishaji bidhaa za ngozi kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Jeshi la Magereza mradi ulioanza mwaka 2017.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Hawa Mchafu amewahimiza watanzania kutumia bidhaa zinazozalishwa Tanzania ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Sambamba na hayo Mchafu amesema matumzizi ya bidhaa za ndani yataongeza soko kwa wazalishaji wa kitanzania na kusaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi hatua ambayo itasaidia kuchangia kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi na kuimarisha maendeleo ya sekta za uzalishaji nchini.
Mwenhekiti huyo alisema hayo Machi 13, 2026 wilayani Moshi mkoa wa Kilimanjaro wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.
Aidha, Mchafu aliongeza pongezi kuwa mradi huo wa kiwanda unatarajiwa kutoa ajira kwa watanzania 3,000 za moja kwa moja na ajira zisizo za moja kwa moja zipatazo 4,00 hatua ambayo itasaidia kuboresha maisha ya wananchi kupitia ajira zitakazozalishwa kiwandani hapo.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amesema kiwanda kina uwezo wa kuzalisha hadi jozi milioni 1.2 za viatu kwa mwaka, soli za viatu jozi milioni 2.1 kwa mwaka na bidhaa mbalimbali za ngozi (leather articles) ikiwemo mikanda, mabegi, pochi, makoti zipatazo 184,500 kwa mwaka.
Sambamba na hayo, Waziri Sangu amesema mauzo yameendelea kuongezeka kila mwaka kutoka shilingi Milioni 936 mwaka 2020/21 hadi kufikia shilingi bilioni 4.0 mwaka ulioshia Juni, 2024/25.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wajumbe wa kamati hiyo,wameipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano kwa juhudi zake za kuendelea kusimamia na kuhamasisha uwekezaji unaolenga kukuza uchumi wa nchi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
MWISHO







0 Comments