THABIT MADAI,ZANZIBAR- MATUKIO DAIMA APP
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barazala Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, amesema, uamuzi wa Serikali wa kushirikiana na Makampuni haya yenye hadhi duniani, utaalamu, uzoefu mkubwa wa uendeshaji na utoaji wa huduma katika Viwanja vya Ndege mbali mbali umesaidia sana kuboresha huduma zetu katika uwanja wa ndege huu na kuuweka katika hadhi ya juu ya viwango vya kimataifa.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa shughuli za DNATA katika jengo la Abiria la Teminal 111 katika uwanja wa Abeid Amani Karume Mjini Unguja.
Alisema, hivi sasa serikali imepata mafanikio makubwa katika uimarishaji wa huduma za Kiwanja cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume, ikiwemo ongezeko la safari za moja kwa moja (direct flights) za Mashirika mbalimbali ya Ndege za Kimataifa.
Alisema hivi sasa Mashirika ya Ndege yapatayo 34 yanafanya safari zake kuja Zanzibar kwa kutumia kiwanja hicho.
“Hivi sasa Zanzibar tunashuhudia ongezeko kubwa la Watalii na Abiria wengine kuja Zanzibar kwa kutumia usafiri wa Anga na kupitia katika Jengo letu la Abiria Terminal 3” alisema.
Alisema katika mwaka 2022, idadi ya Abiria imefikia milioni 1.8 ikilinganishwa na milioni 1.3 kwa mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 38 ambapo ongezeko hilo ni kubwa na halijawahi kutokea.
Aidha lisema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 (Julai – Septemba, 2022), tuliweza kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 6.7. Makusanyo yaliongezeka katika robo ya pili (Oktoba – Disemba, 2022) kufikia shilingi Bilioni 8.1. Hili ni ongezeko kubwa sana ukilinganisha na makusanyo ya robo ya pili mwaka 2019 kabla ya Uviko19 ya Bilioni 2.5.
“Serikali inaelewa umuhimu wa viwanja vya ndege katika kukuza uchumi na kuleta ustawi wa wananchi, Hivyo, tutaendelea kuimarisha miundombinu ya viwanja vyetu vya ndege ikiwemo kiwanja hiki cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume, Kiwanja cha Ndege cha Pemba na Kiwanja cha Ndege cha Nungwi” alisema.
Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi, alisema hivi sasa tayari tunakamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Abiria la Nne (Terminal 4) katika uwanja huu wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume na hivi karibuni Serikali imeingia mkataba na Kampuni ya Propav kwa ajili ya kukiendeleza kiwanja chetu cha Pemba.
Alisema kuwa matarajio ni kukiwezesha Kiwanja cha Ndege cha Pemba nacho kiweze kutumika kwa Ndege za Kimataifa na hivyo kukifungua Kisiwa cha Pemba kiuchumi kama tulivyoahidi ambapo matengemeo kuwa ujenzi wa kiwanja hicho utaanza hivi karibuni.
“Serikali ina nia ya dhati ya kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa Viwanja vyetu vya Ndege pamoja na kutoa huduma bora za abiria na mizigo kwa viwango vya kimataifa jambo ambalo limeanza kuchukuliwa hatua na manufaa yake yameanza kuonekana” alisema.
Pamoja na hayo, alishukuru Wizara, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Makampuni ya Dnata, Emirate Leisure na Segap, na wadau wote wa Sekta ya Anga kwa mashirikiano yao mazuri katika kuimarisha huduma zinazotolewa katika Kiwanja cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume na kusema kuwa imani yake ni wataendelea na jitihada hizo ili tuweze kufikia viwango tunavyotarajia.
Alisema kupitia uwekezaji huo wa jengo la abiria terminal III zaidia ya Vijana 600 wamepatiwa ajira Kwa maslahi yanayolidhisha na kusema kuwa amefurahishwa kusikia kuwa zaidi ya vijana 400 wa kizanzibari ambao wanatoa huduma mbalimbali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume wamepatiwa mafunzo kupitia kampuni ya dnata.
"Mafunzo hayo ni utoaji wa huduma Bora ikiwemo Kwa wateja Kwa hakika huu ni mwanzo mzuri wa kufanya kiwanja chetu kuwa Bora Barani Afrika, kwa kutoa huduma zinazoendana za Kimataifa,"alisema
Hata hivyo, dk Mwinyi, alizitaka taasisi zote ambazo zinafanya kazi katika Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kuendana na viwango vya utoaji wa huduma ambavyo vinatolewa na kampuni ya dnata.
Pamoja na hayo, aliiagiza Idara ya Uhamiaji kazi ya kufanya ikiwemo kupunguza muda wa wasafiri wanaokaa uwanja wa Ndege.
Alisema wakati Sasa umefika Kwa Idara ya Uhamiaji kushirikiana na kampuni ya dnata kuona mfumo upi mzuri wa kietroniki unaofanya kazi vizuri
"Ili wageni wasikae muda mrefu katika Uwanja huu wanapowasili jambo lingine niwatake Mamlaka ya Mapato waongeze bidiii katika shughuli zao kuhakikisha zinakwenda haraka kama inavyotakiwa,"alisema
Mbali na taasisi hizo Rais Dk.Mwinyi amewataka pia watu wa afya na benki zinazotoa huduma kwenye uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Abeid Amani Karume.
Nae, Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano, Dk.Khalid Salum Mohamed alisema mkataba ambao Serikali umeingia na kampuni ya Dnata na kusema utasaidia kuengezeka mapato ya nchi kupitia watalii wanaoingia nchini.
Hivyo, aliahidi kuendelea kushirikiana na kampuni hiyo ili kuona lengo linafikiwa kama ilivyokusudiwa.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Dnata Group, Steve Allen, alisema imani yao uwekezaji huo utasaidia kuleta manufaa na imani yao mashirika ya ndege yataweza kufika Zanzinar na kuhakikisha ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya utalii ambapo itarahisisha uingiaji wa watalii wengi Zanzibar.
"Mbali na faida ya uingiaji wa watalii pia itarahisisha shughuli za kibiashara za uingizaji wa bidhaa mbalimbali kutoka nje ya Zanzibar,"alisema
Pia, alisema uwekezaji huo wa kampuni ya dnata imetoa fursa nyingi za ajira kwa wazawa.
Alisema dnata inahaihakikishia serikali kuwepo kwa uhakika wa usalama katika safari za anga zinazofanyika katika Uwanja huo wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana alisema kupitia uwekezaji uliofanywa na Serikali katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa kujenga jengo la abiria la terminal III uchumi wa Zanzibar utaendelea kukua.
Alisema serikali ya Mkoa itaendelea kuhakikisha kuwa uwekezaji huo uliofanywa utakuwa na ulinzi wa kutosha kupitia kamati ya ulinzi na usalama wa Mkoa.
0 Comments