NA GIFT MONGI,MATUKIO DAIMA APP,MOSHI.
Wadau wa maendeleo mkoani Kilimanjaro wameiomba serikali kupitia wakala wa barabara nchini (TANROADS)kushughulikia Kwa haraka barabara ambazo zipo katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025.
Akizungumza katika kikao cha ushauri mkoa wa Kilimanjaro mbunge wa Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi amesema kuwa kuna baadhi ya barabara ambazo zipo kwenye ilani ya uchaguzi lakini bado zinaonekana kusuasua.
Amesema ipo barabara ya Gate Fonga -Mabogini kwa mara kadhaa imekuwa ikipigiwa kelele lakini bado haijajengwa jambo linaloleta adha kwa wakazi wa maeneo hayo kwa muda mrefu sasa.
"Tatizo kubwa la watu wanaoishi katika jimbo la Moshi vijijini ni barabara viongozi wa mkoa niwaombe mlibebe jambo hili Kwa uzito wake ili kurahisisha shughuli za wananchi wetu tafadhali"amesema Prof. Patrick Ndakidemi
Aidha ameongeza kuwa barabara zote zinazopeleka watalii mlima Kilimanjaro zipo katika hali mbaya hivyo ni vyema fedha za mlima huo zikaelekezwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa ili zielekezwe katika ujenzi wa barabara zinazoenda mlimani.
Mbunge wa Moshi Mjini Priscus Tarimo amesema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakipigia kelele upanuzi wa barabara ya Sokoine(YMCA-KCMC)ipanuliwe ili hakuna kinachofanyika hadi sasa licha ya kuwa barabara hiyo ni muhimu sana.
Amesema katika maeneo ambayo barabara hiyo inapita kuna vyuo vikuu na hospitali ya rufaa ya KCMC hivyo mahitaji ya barabara hiyo ni makubwa kutokana na msongamano uliopo.
Meneja wa wakala wa barabara mkoa wa Kilimanjaro mhandisi Motta Kyando amesema kwa sasa kuna miradi ambayo inatekelezwa na kuwa miradi itaenda kuongezeka kadri ya fedha zinavyoenda kupatikana.
"Barabara ya Same hadi Njiapanda imeshamaliza muda wake hivyo inahitaji marekebisho lakini hata kutoka Njiapanda hadi Moshi hali kadhalika sasa mkandarasi ndio anafanya marekebisho"amesema
Amesema ufungaji wa taa katika mji mdogo wa Bomang'ombe Kwa sasa hautaweza kufanyika kwani kuna ujenzi wa barabara inayotoka Arusha hadi Holili na hivyo kufungua taa sasa zitawaingiza kwenye hasara pindi ujenzi huo utakapoanza.
0 Comments