Header Ads Widget

DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050 KUKAMILIKA ,KUZINDULIWA NA RAIS SAMIA JULAI 17

 

Na Hamida Ramadhan Dodoma

TUME ya Taifa ya Mipango imetangaza kukamilika kwa mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, nyaraka muhimu itakayotoa mwelekeo wa maendeleo ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.

Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Dkt. Fred Msemwa, amesema Dira hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla itakayofanyika Julai 17, 2025, jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 15, 2025, jijini Dodoma, Dkt. Msemwa alisema maandalizi ya Dira hiyo yamechukua karibu miaka miwili, yakihusisha ushirikishwaji mpana wa wananchi kutoka makundi mbalimbali.

“Tulipokea maoni kutoka kwa Watanzania takribani milioni 1.174 kupitia njia mbalimbali, na zaidi ya watu 20,000 walihudhuria makongamano ya kitaifa yaliyolenga kuibua maono ya pamoja kuhusu mustakabali wa Taifa letu,” alisema Dkt. Msemwa.

Aidha, alieleza kuwa Tume ilifanya utafiti wa kina kwa nchi zilizofanikiwa kufikia uchumi wa kati ili kujifunza mbinu bora zinazoweza kutumika katika kufanikisha malengo ya Tanzania, hususan kujenga uchumi wa kati kwa njia endelevu.

Rasimu ya Dira hiyo ilirudishwa kwa wananchi kwa ajili ya uhakiki wa mwisho, kuhakikisha maoni yao yamezingatiwa. Baadaye, nyaraka hiyo ilijadiliwa na makundi ya kijamii, sekta binafsi, na wataalamu, ili kuhakikisha inawakilisha matakwa ya Taifa kwa mapana.

Dkt. Msemwa alibainisha kuwa utekelezaji rasmi wa Dira ya 2050 utaanza Julai 2026, mara baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2025.

Kwa mujibu wa Dkt. Msemwa, Tume ya Taifa ya Mipango inaendelea kusimamia kwa karibu maandalizi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya muda mrefu ili kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo shirikishi, jumuishi na endelevu kwa wananchi wote.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI