Header Ads Widget

WAKULIMA WA KOROSHO WAASWA KULINDA UBORA WA KOROSHO ZAO.

NA HADIJA OMARY, LINDI

IKIWA  Msimu wa mauzo wa zao la korosho ukielekea ukingoni na mvua zikianza kunyesha  wakulima wa zao hilo wanaohudumiwa na Chama kikuu cha ushirika cha (RUNALI) kinachojumuisha wakulima wa Wilaya za Ruangwa Nachingwea na Liwale Mkoani Lindi wamekumbushwa  kuanika korosho zao kabla ya kupeleka kwenye maghala ili ziendelee kuwa na ubora 


Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika RUNALI Odasy Mpunga wakati wa mnada wa tisa wa zao hilo uliofanyika katika makao makuu ya  chama hiko Wilayani Nachingwea Mkoani Lindi 


Mpunga alisema kuwa kwa kuwa hivi sasa msimu wa mvua umeanza wakati bado wakulima wanaendelea kuokota korosho zao na kuzipeleka kwenye maghala ipo changamoto ya uwepo wa unyevu kwenye korosho hivyo ili kuhakikisha ubora wa korosho unaendelea kuwepo ni muhimu kwa wakulima kuanza kuanika korosho zao kabla ya kuzipeleka kwenye maghala .


Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha msingi Makina AMCOS kilichopo wilayani Nachingwea Kasmu Lada alisema viongozi wa vyama vya msingi  Amcos ili kuhakikisha wanaendelea kulinda ubora wa korosho wanazozikusanya wamejipanga kuhakikisha korosho zinazopeleka kwenye maghala makuu zinakuwa safi na salama


Lada aliongeza kuwa  ili kuhakikisha korosho zote zinazopokelewa katika vyama vya msingi zinakuwa hazina unyevu  viongozi wa AMCOS wanazikagua korosho kabla ya kuzipima ili kujiridhisha na ubora wa korosho za mkulima  kwa ajili ya kupeleka kwenye ghala kuu


" kikubwa mkulima akishaleta korosho tunachokifanya ni kumimina zile korosho yaani kwa sasa huwezi kupokea korosho  ukazitia kwenye gunia moja kwa moja , unatakiwa uzimwage, uzikague ukikutana na changamoto unamuambia mkulima azianike zaidi ya siku mbili au tatu halafu ndio unazipeleka ghalani" alifafanua 


Nae mkulima wa korosho kutoka chama cha msingi Nambambo AMCOS Nurudini Mussa alitumia fursa hiyo kukishukuru chama kikuu cha RUNALI kwa kuendelea kusimamia malipo ya wakulima wa zao hilo kulipwa kwa wakati ambapo anasema kuwa licha ya bei ya zao hilo kuwa ndogo lakini viongozi wamekiwa wakijitahidi kuharakisha malipo kwa wakulima jambo ambalo linawafanya waendelee kuwa na imani na chama chao.


Katika mnada huo zaidi ya kilo milioni 3 ziliuzwa kwa bei ya juu ya shilingi 1960 na bei ya chini 1850 ambapo makampuni 12 yalijitokeza kuomba kununua korosho hizo huku mahitaji yakiwa zaidi ya kilo milioni 7.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI