Shirika lisilo la kiserikali la Afyaplus kupitia mradi wa maabara ya hedhi salama, unaolenga kuondoa vikwazo vinavyomkumba binti wakati wa hedhi anapokuwa shuleni. Mradi huu unatekelezwa katika mkoa wa Iringa na kufikia mabinti 30600 kutoka katika shule 50 za mkoa wa Iringa. Shirika limefanikiwa kuanzisha maabara za hedhi salama katika shule 15 kati ya shule 50 za mkoa wa Iringa na kukabidhi mashine 75 na malighafi za kutengeneza taulo za kike za kufua.
Akitoa taarifa ya mradi huo wakati wa kukabidhi mashine hizo jana, mkurugenzi wa shirika la Afyaplus Suzan L. Yumbe, alisema kutokana na tafiti zilizofanywa na mashirika mbalimbali ikiwemo shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) na SNV, ilionekana kwamba watoto wa kike wengi wanashindwa kwenda shule kwa kipindi cha siku kati ya siku tatu hadi tano kutokana na ukosefu wa fedha za kununulia taulo za kike pamoja na kukosekana kwa maji mashuleni.
Hivyo kutokana na changamoto hiyo shirika limeona njia pekee ya kumsaidia mtoto wa kike kusoma kwa raha wakati wote ni kuja na mkakati wa kusaidia upatikanaji wa taulo za kike wakati wote awapo shule kwa kuanzisha maabara za hedhi salama zitakazotengeneza taulo za kike za kufua na kugaiwa bure kwa mabinti wanapokuwa shuleni.
“kutokana na mkakati huo Afyaplus tumeamua kuanzisha maabara 15 kati ya shule 50 za mradi na kutoa mashine 5 kwa shule ili kuanza kuzalisha taulo za kike mashuleni kwa lengo la kumwezesha mtoto wa kike kuwepo darasani wakati wote wa siku zake.”
Sambamba na hilo Mkurugenzi wa shirika la Afyaplus anatoa shukrani zake za dhati kwa serikali ngazi ya taifa hadi wilaya kwa kutoa baraka za kutekeleza mradi huu mashuleni ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufaulu wa Watoto wa kike wakiwemo wale waliokuwa wanashindwa kuhudhuria masomo /vipindi wakati wa siku zao.
Mgeni rasmi katika hafla hii fupi Mhe.Martha Luambano aliyemwakilisha Afisa Elimu wa mkoa Iringa amelipongeza shirika kwa kutoa Elimu Pamoja na vifaa vitakavyosaidia kuondoa changamoto za hedhi kwa Watoto wa kike wanapokuwa shuleni na kuokoa afya zao kwa kuwaepusha na madhara yatokanayo na matumizi ya vifaa ambavyo si salama.Aidha mgeni rasmi aliwasisitiza wakuu wa shule kuhakikisha mashine zilizokabidhiwa zinatunzwa na kufanya kazi tarajiwa.
Kwa upande wake mwalimu wa afya wa shule ya sekondari ya Ipogolo ya Iringa,Ndugu.Munira Mbaruki alisema maabara hizi zilizoanzishwa na shirika la Afyaplus zitakuwa ni Ukombozi Mkubwa katika kuondoa changamoto za hedhi awapo shuleni na kuwafanya mabinti kutumia muda mwingi kufuatilia masomo yao.
Hivyo aliomba wadau wengine kuendelea kujitokeza kumsaidia mtoto wa kike kuondokana na changamoto za hedhi wawapo shuleni.
0 Comments