HALMASHAURI za Mkoa wa Pwani zimetakiwa kutambua vyanzo vyote vya mapato ili wapange bajeti za maendeleo zenye uhalisia.
Aidha zimetakiwa zihakikishe zinatatua migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato.
Hayo yalisemwa Chalinze Wilayani Bagamoyo na Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Zuwena Omary wakati wa kikao cha Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Pwani.
Omary alisema kuwa Halmashauri ikivitambua vyanzo vyote vya mapato itakuwa rahisi kuandaa bajeti itakayokuwa na uhalisia.
"Kazi kubwa ya Halmashauri mbali ya kuleta maendeleo kazi yake nyingine ni kukusanya mapato ambayo ndiyo yanayosaidia kuleta maendeleo kupitia miradi mbalimbali,"alisema Omary.
Alizitaka Halmashauri kubuni miradi mikubwa ambayo ina tija kwa wananchi kuliko kuwa na miradi midogo ambayo haina faida kwa wananchi na Halmashauri.
Naye Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Pwani Juma Ligomba alisema kuwa Halmashauri zipange bajeti zitakazo akisi makisio yao ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali
Ligomba alisema kuwa ili kufikia malengo kila mtu atimize wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi ambao wanategenea viongozi wao kuwaonyesha njia ya kupata maendeleo.
Wajumbe wa kamati hiyo Jumuiya ya Serikali za Mitaa walitembelea soko la Chalinze na stendi mpya ya Chalinze ambavyo vimejengwa kwa mapato ya ndani.
0 Comments