Na Shomari Binda-Musoma
MKUU wa Wilaya ya Musoma, Halafu Haule, amefungua bonanza la michezo katika kuelekea kuazimisha miaka 61 ya Uhuru.
Akifungua bonanza hilo linaloshirikisha timu 4 za Musoma veteran, Biashara United veteran, Watumishi manispaa na TTCL, amesema michezo ni sehemu ya afya na kuweka mwili vizuri kwa kufanya kazi.
Amesema inapoazimishwa miaka 61 ya uhuru kila mmoja anapaswa kuwa na afya njema ambayo inatokana na kufanya michezo.
Haule amesema wilaya ya Musoma katika kusherehekea miaka hiyo 61 ya uhuru michezo pia wameipa kipaumbele kabla ya kufanya matukio mengine kama wilaya.
Amesema licha ya kuitumia michezo kuweka mwili vizuri kiafya amewataka washiriki wote kuitumia kujenga mahusiano.
" Michezo ni sehemu ya kujenga afya na kuongeza mahusiano naomba tuitumie vizuri na tucheze pasipo kuumizana ili tusherehekee vizuri sherehe hizi.
" Tumeandaa zawadi kidogo kwaajili ya mshindi wa kwanza kiasi cha shilingi laki moja na nusu na mshindi wa pili shilingi laki moja",amesema Haule.
Amesema licha ya bonanza hilo wilaya ya Musoma katika kusherehekea miaka 61 ya uhuru imeandaa pia mashindano ya insha kwa shule za msingi na sekondari.
Katika kusherehekea sherehe za miaka 61 ya uhuru mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,ameagiza kiasi cha zaidi ya milioni 900 zilizotengwa kwaajili ya sherehe hizo zitumike kujenga mabweni ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kila wilaya ifanye sherehe hizo.
0 Comments