Na THABIT MADAI, ZANZIBAR- MATUKIO DAIMA APP
IMEELEZWA kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar SMZ kwa Kushirikiana na Wadau mbalimbali wameokoa jumla ya Wahanga 150 wa Usafirshaji Haramu wa Binadamu kwa Kipindi cha Mwaka Mmoja katika bandari Malindi Mjini Unguja.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar Abdallah Saleh Omar wakati akizungumza na Waandishi wa habari alisema kwamba, hatua ni pamoja na kuwepo kwa mradi kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo.
Alieleza kuwa Mradi huo umewezesha kuweka maafisa katika Bandarini pamoja na Viwanja vya Ndege ambapo jumla ya Wahanga 150 wameokolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.
Aliongeza kuwa, tatizo la usafirishaji wa binaadamu bado limekuwa na hali mbaya ambapo kwa asilimia 90 ya wahanga hao ni watoto na wasichana ambao wanatoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na kufika Zanzibar kwa ajili ya kazi za ndani.
Alisema kumekuwepo kwa madalali wengi ambao wanawatoa watoto na wasichana hao kuwaleta Zanzibar kwa ajili ya kazi za ndani ambapo baadhi yao hukumbana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, mateso na manyanyaso.
Alisema kwa sasa Idara inachukua hatua za kuwaunganisha na jamaa zao na kuwarejesha walipotoka kwa kuwagharamia nauli pamoja na chakula wakati wote wa safari.
Hivyo, aliwataka wannachi, wazazi na walezi kuwa karibu na familia zao na kuacha tabia ya kumuamini mtu na badala yake watoto wamekuwa wakitumilishwa na pia hukosa haki zao za msingi.
Mwenyekiti wa Mtandao wa kitaifa wa kuzuwia usafirishaji haramu Tanzania, Edwini Mgambila, alisema hali ya usafirishaji haramu nchini sio nzuri kama zilivyo nchi zingine ambapo kuna vitendo vilivyokithiri kwa wasichana wa kazi za ndani kuchukuliwa mkoa mmoja na kwenda mkoa mwingine au nje ya nchi.
Alisema wasichana hao hupitia katika manyanyaso na mateso makubwa wanapotumikishwa bila ya kupewa ujira na wingine hupoteza maisha, huathirika kiafya ambapo baadhi yao hupata maradhi ya ngono.
Aidha alisema usafirishaji haramu wa ndani ni mkubwa zaidi kuliko wa nje ya nchi na maeneo yanayoongoza ni maeneo ya kazi za ndani, sekta ya ngono kwa kushirikishwa katika kazi za saluni ikiwemo kufanya masaji, sehemu za starehe na sekta za uzalishaji kama sekta ya uvuvi na viwanda.
Hata hivyo, alisema sababu kubwa ya biashara hiyo kunawiri duniani ni thamani iliyonayo na takwimu za serikali ya marekani ya ripoti ya mwaka 2021 inaonesha kuwa biashara ya usafirishaji haramu ya binadamu inawatengenezea wanaofanya biashara hiyo zaidi ya dola bilioni 150 kwa mwaka.
Hivyo, alisema serikali imechukua jitihada mbalimbali na kwa sasa sheria ya usafirishaji haramu wa binadmau imepewa meno zaidi na adhabu kali ikiwemo adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kumsafirisha mtu mzima na kumsafirisha mtoto au mtu mwenyeulemavu ni kifungo cha maisha.
Kwa upande wake Ofisa Muandamizi wa sekretariet ya kuzuwia na kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu katika Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Ahmad Said Mwindad, alisema kwa Tanzania hakuna mkoa ambao upo salama katika usafirishaji huo kutokana na wahanga wanaokolewa.
Alisema kuna sababu mbalimbali zinazopelekea usafirishaji haramu wa binadamu, ikiwemo umasikini na mbinu zinazotumika ni za ulaghai watu wanaahidiwa ujira mkubwa wa kazi ambazo waliahidiwa kupewa.
Alisema sababu zingine ni uelewa mdogo kwa jamii kuhusu wa usafirishaji haramu wa binadamu na ndoto ya kubadilisha maisha kwa kutegemea kazi zenye mshahara mkubwa.
Alisema ili kudhibiti hali hiyo ni vyema jamii kuendelea kupatiwa elimu na kufahamu mbinu zinazotumika za ulaghai na elimu kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kugundua mitandao ya kihalifu inayojihusisha na biashara hiyo na wanaohusika kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
0 Comments