Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar Rahma Kassim Ali amesitisha ujenzi wa michezo ya baharini (Water Sports) unaojengwa na Mwekezaji NJ Water sports eneo la fukwe za bahari Matemwe Wilaya ya Kaskazini ‘A’’ kwa madai ya kukiuka kanuni na sheria ya Ardhi.
Agizo hilo amelitoa mara baada ya kufanya ziara katika eneo hilo ambalo linadaiwa kuwa na mgogoro wa ardhi baina ya Mwekezaji NJ Water Sports na Matemwe Bangaloes ambapo kesi ya mgogoro huo imeshafikishwa Mahakama ya Ardhi Gamba Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja.
“Nimelazimika kusitisha ujenzi unaoendelea ili kuweza kutafutia ufumbuzi mgogoro huo ikiwa ni msimamizi mkuu wa masuala ya ardhi" sitoweza kuacha ujenzi uendelee wakati kesi iko mahamani alisema Waziri huyo.
Alisema Mahakama ya Ardhi Gamba imeshatoa maamuzi ya kusimamisha ujenzi wa mwekezaji NJ Water Spots ambae anadaiwa kuingia eneo la mwekezaji mwenzake huko Matemwe.
Alifahamishwa kwamba Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi haina nia mbaya ya kumuonea mtu bali inahitaji wananchi wafuate sheria ili kuepusha migogoro ya Ardhi inayojitokeza katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Aidha Waziri huyo alitoa wito kwa wageni na wenyeji ambao wanaohitaji kuwekeza ujenzi wa aina yeyote kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu zilizowekwa ikiwemo kupata kibali cha ujenzi kutoka Taasisi ya Utoaji wa vibali vya Ujenzi(DCU) kabla ya kuanza hatua ya ujenzi huo.
Naye Mkurugenzi Mipango Miji na Vijiji Kutoka Kamisheni ya Ardhi Muchi Juma Ameir alifahamisha kuwa lengo la kuwepo kwaTaasisi hiyo ni kuepusha migogoro ya ardhi isiyo na ulazima kwani inarudisha nyuma jitihada za kuleta maendeleo ya nchi yetu.
‘’Kibali ambacho kinatolewa na DCU huwa kinaonesha michoro ya ujenzi katika eneo husika na mipaka, hivyo vibali vya wawekezaji hao vitaonesha mpaka wa kila mmoja” Alisema Muchi.
Naye Mwekezaji Matemwe Bangaloes alisema Mwekezaji NJ Water Sports amejenga ukuta katika eneo lake na hivyo kumtaka avunje ukuta huo kwa muda wa miezi sita ndipo alipoamua kwenda Mahakamani kumshtaki ili apate haki yake.
Kwa upande wake Mwekezaji NJ Water Sports alisema kuwa alifuata taratibu zote kabla ya kuanza ujenzi huo na yuko tayari Serikali ichukuwe hatua za kupima tena michoro ya ujenzi na endapo atakuwa ameingia katika eneo la mwekezaji mwenzake basi yuko tayari kuliachia eneo ambalo limeingia upande wake au kulinunua ili aendelee na ujenzi wa michezo ya baharini.
Mgogoro huo ulianza mwezi wa June, 2022 baada ya NJ water kujenga ukuta katika eneo linalodaiwa sio la kwake hali ambayo imepelekea viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa Ardhi, Rahma, Mkuu wa Mkoa Kaskazini, Ayoub, Mkuu wa wilaya Sadifa, watendaji wa wizara mbali mbali kuingilia kati na mahakama kusimamisha ujenzi huo.
0 Comments