NA HADIJA OMARY,LINDI
MKUU wa Mkoa wa Lindi BI. Zainab Telack amewataka Waganga wakuu wa Wilaya ma DMO kusimamia kwa karibu ujazaji wa kadi alama (SCORE CARD ) za hali ya Lishe kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya sambamba na utoaji wa Elimu ya Lishe kwa akinamama wajawazito na watoto wachanga.
Bi Zainab ametoa Wito huo hivi karibuni wakati wa kikao cha Tathimini na kusaini mkataba wa lishe na Wakuu wa Wilaya za mkoa huo uliofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Telack alisema ujazaji wa chati hizo za lishe kutoka katika vituo vya kutolea huduma za Afya ni muhimu kwa kuwa kutaonyesha hali halisi ya lishe ndani ya Mkoa huo .
“Ma DMO na wataalamu wote waliokuwa kwenye vituo, pale ambapo tunasema wajawazito wapewe vidonge kwa nini tusiwape na tukiwapa kwa nini tusijaze , Watoto wenye uzito pungufu wametibiwa wapo lakini waliokuwepo kwenye vituo hawachukui hizo takwimu, matokeo yake tunajikuta hatuna takwimu lakini Watoto wametibiwa.
“Tujitahidi wale waliopewa dhamana ya kusimamia vituo hakikisheni kila wiki mnaona viashiria vyote ambavyo vinatakiwa kuwepo kwenye chati ya lishe kama vimefanyiwa kazi vizuri na kadi imejazwa” alisema Telack.
Kuhusu Elimu ya Lishe kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya Telack alisema elimu hiyo inapaswa kutolewa kliniki kwa akina Mama wajawazito na Watoto wachanga kabla hawajapimwa.
“Wazazi hawa wanahitaji kupata elimu ya Lishe, mwingine anampa mtoto wake kile anachokiona bila kujua madhara yake mradi mtoto ashibe sasa wataalamu tusaidieni ,hata kule kwenye vituo vya afya ma DMO tukawa na orodha ya vyakula kwamba mama akimpa mtoto wake hiki na hiki itakuwa sasa lishe imekamilika’’ alisema Telack.
Bi Telack aliongeza kuwa Mkoa huo wa Lindi unachangamoto ya wazazi kuwapa chakula Watoto wadogo ndani ya siku moja ama mbili baada ya kuzaliwa.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo mratibu wa lishe mkoa wa Lindi Lewise Mahembe alisema mkataba huo wa Lishe umekuwa ukitekelezwa Nchini kuanzia tarehe 19 Desemba 2017 ambapo Waziri wa Nchi ofisi ya Rais OR Tamisemi kupitia mamlaka za Serikali zitasimamia utekelezaji wa viashiria vya mkataba wa Lishe ili kuboresha hali ya Lishe ya wananchi.
Hata hivyo alisema wakati mkataba huo ukiwa bado unaendelea kutekelezwa lakini bado kunachangamoto ya kubadilishwa kwa matumizi ya fedha za afua za Lishe kwenye halmashauri za mkoa huo na kupelekwa katika matumizi mengine hali inayokwamisha utekelezwaji wa mkataba huo.
Aidha katika wasilisho hilo Mahembe alieza kuwa katika kadi alama (SCORE CARD) ya lishe kwa kipindi cha julai hadi Septemba mwaka 2022 inaonyesha kwa wastani Mkoa wa Lindi unarangi nyekundu.
“Moja ya sababu iliyotupelekea kuwa katika rangi nyekundu ni ulaji wa chumvi isiyo na madini joto kwa baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Lindi pamoja na halmashauri ya nachingwea kushindwa kabisa kujaza kadi alama (SCORE CARD) katika robo hiyo”. alisema Mahembe
Kwa mujibu wa chapisho la Taasisi ya chakula na lishe Tanzania la julai 2019 linaeleza umuhimu wa lishe kwa mama mjamzito kkuwa lishe bora wakati wa ujauzito ni muhimu sana kwa sababu humpatia mama virutubisho muhimu kulingana na hali yake.
Wakati wa ujauzito mama anahitaji virutubisho Zaidi kwa ajili ya maendeleo yake na kiafya pamoja na mtoto aliyetumboni kwani lishe bora huimarisha afya ya mama na humsaidia mtoto kukua vizuri kimwili na kiakili.
0 Comments