Umoja wa mitume na manabii Tanzania tawi la Iringa wametoa
msaada kwa wafungwa wa gereza la Iringa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki
ya manabii na mitume yanayoendelea nchi nzima.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Mwenyekiti wa
umoja huo Bishop Doctor Samwel Shayo amesema wao kama umoja wa mitume na
manabii wameguswa na kupelekea kutoa msaada wa majora matano(5) kwa ajili ya sare
za wafungwa yenye thamani ya Shilingi Milioni Moja.
Pia amesema wamekusanyika toka siku ya Alhamisi katika
ukumbi wa CCM Mkoa wa Iringa kwenye kongamano na mafundisho kwa ajili ya kuelimisha
jamii na maombezi na dua katika kuelekea siku ya Jumapili ambapo kutakuwa na
maombi maalum ya kuiombea nchi, kumuombea Rais na Serikali kwa ujumla, na mgeni
Rasmi katika kuhitimisha kongamano hilo ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Halima
Dendego.
Nae Mkuu wa Gereza mkoa wa Iringa Mratibu Daniel Mwakapila ameshukuru
kwa msaada huo huku akitoa rai kwa jamii kutoa misaada kwa wafungwa maana wanauhitaji
na wengine wametengwa kabisa na jamii zao, ameongeza kuwa misaada hiyo
inasaidia kuwafanya wafungwa warekebike maana wanajiona bado jamii ipo pamoja nao,
hivyo basi inawafanya wabadilike.
Mchungaji Judith Reuben Sanga ambaye ni mjumbe wa umoja wa
Mitume na manabii ametoa rai kwa wanawake kutoa misaada kwenye magereza maana
waliopo magerezani sio kwamba wote wamekosea wengine walisingiziwa, wengine
wameonewa kwa sababu mbalimbali, hivyo basi ameiomba jamii kuwakumbuka wafungwa
maana kwa kufanya hivyo inawafanya waweze kubadilika na wasijione waliotengwa
na kupelekea kurekebika kitabia.
Nae Mchungaji Getruda Eyamba ambaye ni Mweka Hazina wa umoja
wa mitume na manabii amesema wajibu wao ni kuwapenda maana “Mungu mwenyewe ni
upendo” na kuwaombea ili waweze kujua wanayoyafanya sio mazuri waweze
kubadilika na kuishi kwa kumtegemea Mungu.
Doctor Amos Ponella yeye ni Katibu wa umoja wa Mitume na
manabii amesema wajibu wao ni kuelimisha jamii katika maeneo mbalimbali ili
jamii iweze kuepukana na ukatili wa kijinsia kwa sababu jambo hilo linaliathiri
taifa na linaharibu nguvu kazi ya taifa kwa hiyo wao kama viongozi wa dini
wanatoa elimu kwa kadiri wanavyoweza na ameitaka jamii kukataa na kupinga ukatili wa kijinsia kwa sababu pasipokufanya hivyo kinaandaliwa kizazi kibaya cha watanzania.
0 Comments