Header Ads Widget

KAMPUNI YA MANTRA TANZANIA ROSATOM YATOA MSAADA WA VIFAA VYA UJENZI KATIKA KATA YA LIKUYUSEKA -NAMTUMBO.

                                            Meneja uhusiano mantra Khadija Kawawa
                                               Diwani kata ya Likuyuseka Kasimu Gunda
Rajabu Nyoni akizungumza kwa niaba ya wananchi wakati wa kupokea msaada wa vifaa vya ujenzi katika kata ya Likuyuseka Namtumbo
Wananchi wakipokea bati 140 zilizotolewa na kampuni ya Mantra Tanzania Rosatom
                                xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Na Amon Mtega, Namtumbo.

KAMPUNI ya Mantra Tanzania Rosatom inayojishulisha na madini ya Uranium katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma imetoa msaada wa Vifaa vya ujenzi kwenye kata ya Likuyuseka ili kufanikisha kukamilisha ujenzi wa majengo yanayojengwa kwa nguvu ya Wananchi katika kata hiyo.


 Akizungumza Meneja uhusiano wa kampuni ya Mantra Tanzania Khadija Kawawa wakati akikabidhi vifaa hivyo vyenye thamani zaidi ya shilingi Milioni Saba (Sh.7,000,000) amesema kuwa kampuni hiyo imetoa msaada huo ili kuunga mkono jitihada za maendeleo ya Wananchi wa kata hiyo na Wilaya nzima kwa ujumla wake.


Meneja uhusiano huyo amefafanua kuwa msaada huo umetolewa katika Vijiji vitatu vya kata ya Likuyuseka ambapo Kijiji cha Mtonya kimesaidiwa bati 140 za geji 28  na misumali zaidi ya kilo 200 kwaajili ya kuezekea ofisi ya Kijiji hicho ambayo tangu kianzishwe mwaka 1977 hakijawahi kuwa na ofisi ya Kijiji.



Akizungumzia vifaa vingine kuwa vimetolewa katika Kijiji cha Likuyusekamaganga Saruji na Kokoto kwaajili ya ya kumalizia ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya Msingi ya Likuyusekamaganga ambayo yamejengwa kwa nguvu za Wananchi.


Aidha katika Kijiji cha Mandela kampuni hiyo imetoa Kokoto na usafiri wa kubebea tofali kutoka zilikofyatuliwa hadi kwenye ujenzi wa jengo la mama na mtoto linalojengwa kwenye kituo cha Afya kijijini hapo.



 Kawawa amesema kuwa licha ya kampuni hiyo kutoa misaada hiyo kwa kutambua nguvu za Wananchi lakini bado kampuni hiyo inaunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea maendeleo Wananchi wake ambapo hadi sasa miradi mbalimbali imefanyika na inaendelea kufanyika.


 Kwa upande wake diwani wa kata ya Likuyuseka Kasimu Gunda akipokea msaada wa Vifaa hivyo amesema kuwa anaishukuru kampuni ya Mantra Tanzania kwa kujali nguvu za Wananchi wa kata hiyo na kuwa wataendelea kushirikiana na kampuni hiyo katika kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.



Naye mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Mtonya Rajabu Nyoni amesema kuwa hawaamini kupatiwa msaada huo na kampuni hiyo kwa kuwa Kijiji hicho tangu kuanzishwa mwaka 1977 hakijawahi kuwa na ofisi yake ambapo hadi sasa kampuni ya Mantra Tanzania imeweza kuwasaidia katika kufanikisha ujenzi huo.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS