Header Ads Widget

BODABODA WAFUNGUKA KUHUSU MIMBA ZA WANAFUNZI



Afisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya Kigoma Minza Edward akizungumza katika mkutano wa kupinga ukatili uliofanyika kijiji cha Kizenga Kigoma Vijijini 



waendesha bodaboda katika kijiji cha Kizenga Kigoma Vijijini wakifuatilia mdahalo wa kupinga ukatili uliofanyika katika kijiji hicho chini ya uratibu wa idara ya maendeleo ya jamii ya halmashauri ya wilaya Kigoma.


(Picha na Fadhili Abdallah)

                         xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

Waendesha pikipiki (bodaboda) katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Kigoma wamesema kuwa wazazi kukwepa majukumu yao ya kuwahudumia watoto wao kwenye masuala ya elimu kumepelekea wanafunzi kuangukia kwenye mikono ya waendesha bodaboda na kupata ujauzito.

 

Hayo yamebainika kwenye mikutano ya uhamasishaji jamii kupinga vitendo vya ukatili mikutano iliyoendeshwa na Maafisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya Kigoma.

 

Mmoja wa waendesha boda boda hao, Jafari Dunia kutoka kijiji cha Kizenga halmashauri ya wilaya Kigoma Akizungumza katika mkutano uliofanyika kijijini hapo alisema kuwa wazazi wamewatelekeza watoto wao kwa kigezo cha hali duni ya maisha na kuwaacha watoto hao wakitanga tanga na kuangukia mikono isiyo salama.

 

Mwendesha boda boda Dominic Simon kutoka kijiji cha Kalinzi halmashauri ya wilaya Kigoma akizungumzia tatizo hilo alisema kuwa waendesha boda boda wanaweza kulaumiwa kwa mimba za wanafunzi lakini tatizo linaanzia kwa wanafunzi wenyewe kushawishi kupewa lifti ya kwenda shule na kutaka pia wasaidiwe na huduma nyingine ikiwemo pesa za chakula.

 

“Kibinadamu inaweza kutokea kwa yeyote kwa sababu huwezi kumsaidia mtu bila kunufaika hasa unapopoteza mafuta na muda wa kumpeleka mwanafunzi shule na wakati mwingine kumgharamia chakula na mahitaji mengine ambayo yalipaswa kufanywa na mzazi, kwa hali hiyo chochote kinaweza kutokea,”Alisema Mwendesha bodaboda huyo.

 

Mwenyekiti wa kijiji cha Kizenga, Juma Tungilayo alisema kuwa serikali ya kijiji imekuwa ikipokea kesi nyingi za waendesha boda boda kuwapa mimba wanafunzi na baadaye kuwakimbia hali inayowafanya wasichana kufukuzwa shule lakini kukosa matunzo ya watoto wao kwa watu waliowapa mimba.

 

Mwenyekiti huyo alisema kuwa tatizo hilo kwa sehemu kubwa linaanzia kwa wazazi wa wanafunzi ambao wanalo jukumu la kuwasimamia, kuwagharamia huduma zote lakini kuhakikisha wanawalinda na mambo ambayo yanaweza kuwaharibia maisha yao lakini wazazi wengi wanakimbia jukumu hilo kwa kigezo cha hali ngumu ya maisha.

 

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Kizenga Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya wilaya Kigoma, Minza Edward alisema kuwa ukatili unaofanywa na waendesha bodaboda una madhara makubwa kwa wanafunzi na watoto wanaozaliwa na wanafunzi hao kwa siku zijazo.

 

Minza alisema kuwa licha ya wanafunzi kuwa na hali ngumu ya maisha lakini kitendo cha kupata ujauzito kinaongeza matatizo zaidi hivyo ametoa wito kwa jamii kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kuwalinda, kuwahudumia watoto wao lakini kushiriki kikamilifu kwenye vita ya kupinga ukatili ikiwemo kuwapa ujauzito wanafunzi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI