Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma
WAZIRI wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu Sara, Bunge na Uratibu Gerorge Simbachawene amesema Uzinduzi wa Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo ya Mwaka 2022 yatafanyika Oktoba 31, Mwaka huu Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dodoma amewataka wananchi mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo
Amesema Oktoba 31 ni siku maalum kwa taifa hivyo basi wananchi wahakikishe wanajitokeza kwa wingi katika viwanja vya Jamhuri huku wale waliombali na Mkoa wa Dodoma kufuatilie uzinduzi huo kupitia vyombo vya habari ili tushiriki pamoja na Mheshimiwa Rais kujua tupo wangapi wakati atakapotangaza Matokeo hayo ya Mwanzo.
"Uzinduzi huo ni tukio muhimu katika historia ya maendeleo ya nchi ndio maana Serikali imeamua kuhakikisha kunakuwa na uwakilishi wa wananchi wa makundi yote ili waweze kushiriki katika tukio hili la kihistoria," .
Na kuongeza "Sensa ya Watu na Makazi hufanyika mara moja kila baada ya miaka kumi na matokeo yake ndio yanayotumika katika kufanya maamuzi yote muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi kwa kipindi cha miaka kumi hadi Sensa nyingine,hivyo
Sherehe hizi za uzinduzi wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 zitahudhuriwa na viongozi wote wakuu wa Serikali pamoja na Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marais wastaafu wa Zanzibar,"alisema Waziri Simbachawene.
Alieleza kuwa katika uzinduzi huo pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Marais hao wastaafu watatunukiwa tuzo maalum kwa kufanikisha Sensa katika vipindi vya uongozi.
Aliwataja Waalikwa wengine kuwa ni viongozi wa Serikali wakiwemo mawaziri na manaibu waziri, Makatibu wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Serikali zetu zote mbili, Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar, viongozi wa vyama vya Siasa na wawakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii.
"Wageni wengine mashuhuri ni pamoja na Waheshimiwa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao humu nchini, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yakiwemo ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika na Wadau wengine wa Maendeleo,"alifafanua Waziri huyo.
Sambamba na hayo alisema katika sherehe hizo, mbali ya kuzindua Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan atazindua pia Mwongozo Maalum wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ambao lengo lake kuu ni kuhakikisha matokeo ya Sensa yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
"Matokeo haya ni muhimu sana kwa makundi yote katika jamii, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji na hasa kwa Serikali yetu inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwani Serikali itaweza kupanga mipango yake kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kulingana na idadi, mahitaji na mazingira wanamoishi,"alisisitiza na kuongeza;
Kwetu sisi wananchi wa Dodoma, hii itakuwa historia kwa kuwa itakuwa mara ya kwanza kushuhudia tukio la uzinduzi wa Matokeo ya Sensa ambao ni fursa moja muhimu kwenu kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia uzinduzi huo ambao utapambwa na kila aina ya shamrashamra kuonesha kuwa sio tu kuwa ni tukio la kihistoiria kufanyika Dodoma pia ni tukio linalitokea mara moja tu kila baada ya miaka kumi,"alisema.






0 Comments