Header Ads Widget

RC KIGOMA AMALIZA TAHARUKI MGOGORO WA KIWANJA BAINA YA KANISA NA JUMUIYA YA WAZAZI YA CCM

Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye akitoa maagizo ya Waziri wa ardhi kuhusu mgogoro wa umiliki wa eneo ilipo chumvi sekondari wilaya ya Uvinza baina ya Jumuiya ya wazazi ya  CCM na Kanisa Katoliki jimbo la Kigoma

                            Mussa Madua Katibu wa idara ya ardhi jimbo Katoliki Kigoma

Katibu wa idara ya elimu na malezi  kutoka Makao makuu ya Jumuiya hiyo Dodoma, Joseph Ludovic 

 Na Fadhili Abdallah,Kigoma

MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amemaliza taharuki ya mgogoro wa kiwanja baina ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma na Jumuiya ya wazazi ya Chama Cha Mapinduzi kuhusiana na uhalali wa umiliki wa eneo ilipo shule ya sekondari ya Chumvi ambapo Mkuu huyo wa mkoa ametaka maagizo ya Waziri wa Ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi Angeline Mabula yatekelezwe.


Katika maamuzi ya Mabula kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa miaka 30 ameitaka Jumuiya ya wazazi CCM mkoa Kigoma inayomiliki shule hiyo kuondoa kila kitu chao katika eneo hilo ifikapo September 12 mwaka huu ili kupisha kanisa katoliki jimbo la Kigoma kumiliki na kuendelea na shughuli zao kwenye hilo.


Baada ya maamuzi hayo ya Waziri kumetokea taharuki kwenye eneo hilo ambapo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Jumuiya ya wazazi ya CCM kuondoka eneo hilo na ndipo September 28 mwaka huu wanaoaminika waumini wa kanisa hilo kigango cha Uvinza kuvamia eneo hilo na kuvunja vyoo wakiwa na mpango wa kuvunja majengo ya shule hiyo.


Hali hiyo ilileta taharuki kubwa kwa wanafunzi wa bweni wa shule hiyo ya Chumvi iliyopo kwenye mji mdogo wa Uvinza wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ambapo kwa karibu wiki mbili sasa wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na matukio hayo.


Sambamba na hilo Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma iliamua kuanzisha kongamano la Berthania la mwaka wa Rozali, kuombea marehemu na kuliweka wakfu eneo hilo kuwa la ibada  ambapo walifunga vyombo vya muziki na kufanya eneo hilo kutokuwa rafiki kwa wanafunzi kujisomea huku kukiwa na hofu ya kuvamiwa na kutokea mapigano.


katika kikao cha pamoja cha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa Kigoma, Viongozi wa kanisa katoliki wakiwakilishwa na mapadre wanne na Katibu wa idara ya ardhi jimbo Katoliki Kigoma huku Jumuia ya wazazi ya CCM ikiwakilishwa na  katibu wa idara ya elimu na malezi  kutoka Makao makuu ya Jumuiya hiyo Dodoma na Katibu wa Jumuiya hiyo mkoa Kigoma.


Katika kuhitimisha mgogoro huo Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema kuwa ameagizwa kutoa maelekezo ya kufuata maagizo ya Waziri wa Ardhi kumaliza mgogoro huu na pande zote zinapaswa kufuata maelekezo waliyopewa na Waziri wa ardhi.


Pamoja na hilo Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa kwa sasa kuna wanafunzi wanafanya mitihani ya kidato cha pili na cha nne hivyo ametoa maagizo kwa pande zote kuhakikisha wanaacha wanafunzi hao wamalize mitihani ya Taifa na baada ya hapo Jumuiya ya wazazi iondoe mali zake na kukabidhi eneo kwa Kanisa katoliki.


Wanafunzi wa kidato cha pili na wale wa kidato cha nne wanatarajia kumaliza mitihani yao hadi kufikia Desemba Mosi mwaka huu.


Akizungumza katika kikao hicho Katibu wa Idara ya ardhi ya jimbo Katoliki Kigoma, Mussa Madua alisema kuwa maagizo ya Waziri inawataka Jumuia ya wazazi kuondoka eneo hilo kufikia September 12 mwaka huu lakini hadi sasa hawajaondoka na wamepewa maelekezo ya kumuona Askofu Mkuu wa jimbo Katoliki Kigoma kama wanataka kuongezewa muda lakini hawakufanya hivyo na ndipo Oktoba 13 kanisa ikaamua kuanza kuendesha kongamano eneo hilo.


Akitoa maelezo kwa niaba ya Jumuiya ya wazazi ya CCM katibu wa idara ya elimu na malezi  kutoka Makao makuu ya Jumuia hiyo Dodoma, Joseph Ludovic alisema kuwa wapo tayari kuondoka eneo hilo lakini maelekezo ilikuwa ni kusubiri wanafunzi wa kidato cha pili na nne kumaliza mitihani yao ya kitaifa na baada ya hapo wataondoka eneo hilo lakini wanashangazwa na hili linalotokea.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS