Na Fatma Ally Matukio Daima APP Dar es Salaam
Chama Cha NCCR- Mageuzi kimesema kuwa licha ya kutopewa nafasi ya kushiriki katika kikosi kazi cha kukusanya maoni kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan lakini sio sahihi kwa baadhi ya vyama kukilalamikia kikosi kazi hicho kwani kilishiriki katika kutoa maoni yake.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti Bara NCCR Mageuzi, Joseph Roman Selasini wakati apokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema wao hawawezi kuchukia kutoshirikishwa katika kikosi kazi hicho kwa sababu chama Chao kulikuwa kinapitia changamoto ya kugawanyika makundi mawili.
"NCCR-Mageuzi tunaiona ahadi ya Rais Samia kushauriana na wasaidizi wake na kufanya mapitio ya baadhi ya sheria kuwa yenye mashiko, kwa mfano sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 inatakiwa kuhuishwa Ili mchakato uanze"amesema Selasini.
Amesema kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan hawezi kurekebisha sheria kwenye mimbari kwani marekebisho ya sheria ni mchakato wa muda mrefu, hivyo ni busara kupewa nafasi na wananchi na baadhi ya vyama vya siasa kuwa na subra badala ya kuamsha mijadala ya shutuma .
"Tunasisistiza maoni ambayo hayana mgogoro wa kisheria wala kikatiba, yasiendelee kunyamaziwa kwa sababu yanazusha mijadala isiyo ya lazima, hivyo Katiba mpya, Tume huru ya Uchaguzi na sheria zinazosimamia uchaguzi Mkuu wa Serikali za mitaa zifanyiwe maamuzi ya haraka Ili kuendana na matarajio ya watanzania katika uchaguzi ujao"amesema Selasini.
Aidha, amesema wanakipongeza kikosi kazi kwa kuwasilisha maoni ya wale waliohojiwa na pia wanampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuyapokea maoni hayo, hivyo mijadala inayoendelea ndani ya vyombo mbalimbali vya habari na baadhi ya vyama vya siasa ni tamaa ya kutaka mtoto azaliwe kabla ya wakati.






0 Comments