Na Amon Mtega,Mbinga
MKUU wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Aziza Mangosongo ameapa kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaohujumu fedha za ujenzi wa miradi ya madarasa kwenye baadhi ya shule zilizoanishwa Wilayani hapo.
Mangosongo amesema hayo wakati wa kikao cha utoaji wa taarifa za ujio wa fedha zaidi ya sh.Milioni 400 za ujenzi wa madarasa 12 ambayo yatajengwa kwa mgawanyo kwa Halmashauri mbili ya Mbinga mji madarasa saba na Mbinga Vijijini madarasa matano.
Mkuu huyo akizungumza kwenye kikao hicho kilichohudhuliwa na Wajumbe mbalimbali wakiwemo na baadhi ya madiwani wa maeneo husika amesema kuwa kumekuwepo kwa baadhi ya watu waliopo kwenye kamati za ujenzi kuingia tamaa ya kuhujumu miradi hiyo kwa lengo la kujipatia fedha jambo ambalo hupelekea baadhi miradi kushindwa kukamilika kwa wakati ni mingine huwa chini ya viwango .
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inajitahidi kutoa fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ya madarasa ili kuwafanya watoto wasome kwenye mazingira bora lakini baadhi yenu mnakwamisha jitihada hizo kwa tamaa ya fedha.
Kwa upande wake Frederick Msae kamanda wa kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mbinga amesema kuwa miradi iliopita baadhi ilikuwa na kasoro nyingi ambazo ofisi yake ilibaini hivyo ni vema wakati wa ujenzi miradi hii mipya taratibu zifuatwe ili kuondoa mkanganyiko.
Hata hivyo Msae amewataka wakurugenzi wa Halmashauri hizo kuwawezesha wahandisi wao ili waweze kufika kwa wakati kwenye miradi inayotekelezwa ili wakatoe ushauri kabla ya kuanza ujenzi .
0 Comments