Header Ads Widget

BIMA YA AFYA KWA WOTE YALENGA MAKUNDI MAALUM YA KIMKAKATI-WAZIRI MCHENGERWA

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa


Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema mpango wa Bima ya Afya kwa Wote umejikita kuyafikia makundi maalum ya kimkakati ikiwemo wafugaji, wakulima, wasanii, waendesha bodaboda na wachimbaji wadogo.

Waziri Mchengerwa ameyasema hayo leo Februari 2, 2026, wakati akizungumza katika kikao kazi na Wahariri wa Vyombo vya Habari kilichofanyika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

Waziri Mchengerwa amesema dhamira kuu ya Serikali ni kumfuata mwananchi popote alipo kwa kutumia lugha na njia zinazoeleweka kwa kundi husika, ili kuongeza uelewa kuhusu Bima ya Afya kwa Wote na kuhamasisha usajili wa wananchi wengi zaidi.





Kwa upande mwingine, amesema mpango huo pia utazingatia makundi yasiyo na uwezo, yakiwemo wazee, wajawazito na watu wenye ulemavu, ambao wataendelea kupatiwa huduma za matibabu bila malipo kwa mujibu wa utaratibu wa Serikali.

Aidha, ameeleza kuwa katika kuhakikisha taarifa za Bima ya Afya kwa Wote zinamfikia kila mwananchi, Serikali itaingiza ajenda ya bima katika shughuli za kila siku za kijamii na kiuchumi, pamoja na kutumia sanaa, wasanii na teknolojia ya habari katika kampeni za uhamasishaji.

Aidha, amebainisha kuwa, Serikali imejipanga vyema ili kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa wote husuasan ni eneo la makundi maalum pamoja na matibabu ya magonjwa sugu ili mwananchi aweze kufurahia huduma za afya nchini.

"Mhe. Rais atakapokwenda kuzindua Bima ya Afya kwa wote atazindua pia mpango wa matibabu ya wale wasiojiweza (wazee na makundi maalum) hasa kwenye matibabu ya magonjwa sugu, sisi kama wizara tumeshajipa na kujiandaa katika utekelezaji," amesema Waziri Mchengerwa.





Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalage, amesema uamuzi wa Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, kuwaita wahariri wa vyombo vya habari katika kikao kazi ni sehemu ya mkakati wa utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mzuri kuhusu masuala ya bima hiyo.

“Baada ya kupata Uhuru, wananchi walikuwa wanapata matibabu bure. Hata hivyo, kadri muda ulivyokwenda na kutokana na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, Serikali ilianza kuweka mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha kila mwananchi anapata matibabu kwa wakati na kwa urahisi,” amesema Dkt. Shekalage

Dkt. Shekalage amesema wanahabari ni wadau muhimu wenye uwezo wa kuhamasisha jamii, kuelimisha na hata kutuliza pale panapokuwa na sintofahamu katika masuala ya msingi, ikiwemo Bima ya Afya kwa Wote. 

Ameongeza kuwa sera ya afya iliyopo sasa inawezesha wananchi wasio na uwezo kupata huduma bora za afya kupitia mfumo wa bima.

“Sera yetu ya afya kupitia Mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote inatoa nafasi kwa wananchi wasio na uwezo kupata huduma bora za afya kwa gharama nafuu katika kipindi chote cha mwaka,” amesema Dkt. Shekalage.

Nae Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF)Deodatus Balile amesema Jukwaa la Wahariri limeshiriki ili kujifunza na kuwafikishia wananchi kuhusu Bima ya Afya kwa wote kupitia TV, Radio na Magazeti kwa wakati mmoja. Kuhamasisha wananchi juu ya usawa katika matibabu kupitia Bima ya Afya.








Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF)Deodatus Balile


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI