Header Ads Widget

MBUNGE WA MOSHI VIJIJINI Prof. PATRICK NDAKIDEMI AHUDHURIA MAHAFALI YA SHULE YA SEKONDARI YA MASOKA.

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI.

Mbunge wa jimbo la Moshi vijijini Prof Patrick Ndakidemi amehudhuria mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Masoka iliyopo katika Kata ya Kibosho Kirima, Jimbo la Moshi Vijijini ambapo aliongozana na Diwani wa Kata hiyo Inyasi Stoki.


Kwenye mahafali hayo Mgeni Rasmi alikuwa ni Mama Esther John Kamalo, ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Akina Mama Kata ya Kibosho Kirima.



Vilevile, walikuwepo wajumbe wa bodi ya shule, viongozi wa madhehebu mbalimbali, wakuu wa shule jirani za sekondari na msingi, wazazi na wageni wengine waalikwa. 


Awali akisoma taarifa kwa mgeni rasmi, Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Masoka Mwl. Ahmed Litinji alisema shule ya Masoka imepiga hatua kubwa kwani watoto wanapata malezi bora kielimu, kimwili na kiroho. 



"Tunawajenga watoto katika maadili mema yanayozingatia haki na uadilifu, na stadi za naisha ili baadaye waje kuwa raia bora kwa Taifa"


Katika mahafali hayo, Shule ilialika viongozi mbalimbali wa dini ambao walifanya maombi maalumu kwa ajili ya watoto.



Akizungumza kwenye mahafali hayo, mgeni rasmi Mama Esther Kamalo  amesema kuwa amefarijika sana kuona kuwa shule ina ufaulu mzuri, kitu kinachoashiria kuwa shule imeimarika ikilinganishwa na miaka ya nyuma.


Mama Kamalo alimpongeza mwalimu mkuu na timu yake pamoja na mwenyekiti wa bodi ya shule na wajumbe wake kwa usimamizi wao makini, ueledi na uaminifu mkubwa.


Umoja huo umewezesha shule hiyo kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kufikia ndoto yake ya kuwa shule kinara katika matokeo ya kidato cha nne kwa wale waliomaliza mwaka wa 2021 kwa shule za serikali katika halmashauri ya Moshi.



Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Akina Mama Kata ya Kibosho Kirima amewataka wazazi na walezi kusimamia malezi ikiwa ni pamoja na nidhamu na maadili kwa kushirikiana na walimu kuhakikisha watoto wanapata elimu iliyokuwa sahihi huku watoto wakitakiwa kuwatii waalimu na wazazi wao na kuzingatia kile wanachofundishwa na walimu wao.


Akizungumza katika mahafali hayo, Mbunge Ndakidemi alisema kuwa ataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa shule hiyo ili iendelee kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.


"Kama mnavyojua, mimi nilikuwa mwenyekiti wa bodi wa shule hii toka ianzishwe baada ya kuwa Mbunge, nimeiacha ikiwa imeshika nafasi ya kwanza kwenye matokeo ya kidato cha nne kwa shule za serikali za halmashauri ya Moshi nawaomba wazazi tuwasaidie walimu ili shule isiporomoke hata kidogo". Alisema Mbunge.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI