Na Matukio daima media , Mbeya
WAUMINI wa kanisa la Kristo lililopo Kata ya Chimala wilayani Mbarali mkoani Mbeya wametoa msaada wa vitu mbali mbali kwa wazee 30 wasiojiweza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wazee Duniani.
Vitu vilivyotolewa kwa wazee hao ni kilo 60 za sukari ,sabuni , blangeti tano , mashuka matano , pamoja na nguo kwa wazee 30 wasiojiweza .
Akizungumza na mtandao huu leo mara baada ya vifaa hivyo kukabidhiwa kwa wazee,Mwenyekiti wa umoja wa wazee Kata ya Chimala,Wily Chenelo kuwa kwa kata ya Chimala pekee wana idadi kubwa ya wazee wasiojiweza ambao wana uhitajhi mkubwa hasa wanawake na mbaya zaidi hawapati TASAF.
Mzee Chenelo alisema kuwa licha uhitaji walionao wazee hao lakini bado wana familia ambazo zinawategemea ambao kwa kiasi kikubwa ni wajukuu ambao wameachiwa na watoto wao na wao kushindwa kuwakumbuka wazee wao.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo aliomba serikali iwaangalie wazee wanaojishughulisha na kilimo wapatiwe ruzuku ya pembejeo ili waweze kupata kwa bei nafuu ilim kila mzee aweze kumudu gharama hizo.
Akizungumzia kuhusu vyeti vya msamaha wa matibabu kwa wazee hawapati hivyo kulazimika kupokea malalamiko ya wazee mara kwa mara kuhusu vyeti hivyo.
“Ndugu yangu mwanangu hali ni mbaya kwa wazee kwani hata huu msaada waliopatiwa kutoka kwa waumini wa Kanisa la Kristo bado hautoshelezi mahitaji ya wazee kutokana na kuwa wengi wazee hao ,hivyo tunaomba watu mbali mbali wajitokeze kusaidia kundi hili la wazee ili wapate mahitaji muhimu hususani nguo , chakula na mahitaji mengine muhimu “alisema.
Kwa upande wake Msaidizi wa Mchungaji wa kanisa la Kristo lililopo kata ya Chimala wilaya ya mbarali ,Meshack Malongo alisema kuwa waliguswa kuwasaidia wazee wasiojiweza kwani Mungu anawahitaji waweze kusaidiwa kutokana na hali halisi ya uzee waliyonayo.
Aidha Malongo alitoa wito kwa makanisa mengine kuwa na ibada iliyo njema kwa kuwaombea wazee wasiojiweza ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wazee wasiojiweza.
“Sisi binadamu kila mmoja ana moyo wake hivyo sisi viozi wa dini tunapaswa kuwaelekeza waumini wetu kujua umuhimu wa kujitoa kwa ajili ya kuwasaidia wazee wetu wasiojiweza kwani wapo wazee wengine hawana uwezo kabisa”alisema kiongozi huyo wa dini .
Kwa upande wake Afisa Ufuatiliaji wa Asasi isiyokuwa ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya wazee (KIWWAUTA) Mussa Mchalo alisema kuwa asasi hiyo imekuwa bega kwa bega na wazee katika kuwasaidia kupitia kwenye mabaraza ya wazee .
Mwisho.
0 Comments