WAKULIMA WA PAMBA WILAYA YA CHEMBA WAPEWA ELIMU YA KILIMO BORA
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA APP
WAKULIMA wa pamba wilayani Chemba mkoani Dodoma wametakiwa kulima zao hilo kwa kutumia vipimo vipya vya kisasa.
Vipimo hivyo ni sentimeta 60 kutoka mstari hadi mstari na sentimeta 30 kutoka shimo hadi shimo na kuacha mtindo wa zamani wa kurusha mbegu.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Aggrey Mwanri kwa nyakati tofauti alipokuwa akitoa semina elekezi ya namna ya kuongeza tija kwa kutumia vipimo vipya katika zao hilo
kwa wakulima wa vijiji vya Kidoka, Ombili, Paranga na Kelema.
Mwanri amesema kuwa mabadiliko hayo ya vipimo yatamwongezea mkulima idadi ya miche kutoka 22, 222 ya awali alipokuwa anatumia vipimo vya sentimeta 90 kwa sentimeta 40 hadi kufikia miche 44,444 kwa kutumia vipimo vipya.
Amesema kuwa endapo wakulima watatumia vipimo vipya wakati wa kupanda zao la Pamba ifikapo mwaka 2025 wanatarajia kuzalisha tani milioni 1 na watakuwa wa kwanza Afrika kwa uzalishaji wa Pamba.
"Kama wakulima wakifuata maelekezo na kanuni bora za kilimo cha zao la Pamba kwa kupanda shamba zima kwa kutumia vipimo na kuachana na mtindo wa kupanda mstari wa mbele kwa kufuata vipimo alafu wanaendelea kumwaga mbegu kama zamani hatutafikia malengo tuliyojiwekea"
Aidha Mwanry ambaye amewahi kuwa kushika nyadhfa mbalimbali serikalini alisema Pamba ni zao muhimu la kimkakati na kibiashara huku pia likichangia takribani asilimia 10 hadi 20 ya pato la Taifa.
Mbali na hayo alisema zao la Pamba pia linaingiza fedha za kigeni sambamba na kutoa ajira kwa asilimia 40 ya Watanzania.
Kutoka na umuhimu huo, alisisitiza kuwa wakulima hawana budi kulima zao hilo kwa kufuata kanuni bora za kilimo ikiwemo kupambana na wadudu waharibifu kwa kutumia viuatilifu.
"Tunapoendelea kutoa elimu, tutaendelea kuwaelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu pamoja muda mwafaka wa kupulizia dawa na vifaa maalumu vinavyotumika wakati wa kunyunyuzia dawa hiyo" alisema Mwanri.
Sambamba na Hayo amefafanua kuwa Bodi ya Pamba tayari imeishachukua hatua mbalimbali ya namna ya kuwasaidia wakulima kupata viuatilifu vitakayowasaidia kupambana na wadudu waharibifu shambani.
"Bahati nzuri taarifa tulizonazo ni kwamba sasa wameishaanza kupata viuatilifu ambavyo vitapambana na funza, chawajani na wadudu wengine waharibifu" alisema Mwanri.
Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Kamili Makiya amesema kutokana na programu ya kuhamasisha kilimo cha Pamba wilaya hiyo imeanza kuwa na matarajio ya kunufaika tofauti na kipindi cha nyuma ambapo zao hilo lilianza kuzorota.
"Kwa mfano ukiangalia takwimu za nyuma jinsi tulivyokuwa tunaendesha kilimo mwaka 2018 -2019 tulifanikiwa kuzalisha tani 111 lakini baada ya miaka hiyo tukaachana na programu ya kuhamasisha mara kwa mara na uzalishaji ulishuka chini 2019-2020 tulizalisha tani 73 mpaka kufikia 2020_2021 tulipata tani 500 kwa mwaka" alisema Kamili.
John Joseph na Shabani Hassani ni baadhi ya wakulima waliopata elimu elekezi namna ya kuongeza tija kwenye zao la Pamba wamesema kuwa elimu hiyo itawasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya mabadiliko katika zao hilo, na kuiomba bodi ya Pamba kuendelea kutoa elimu namna ya kuendelea kutumia Vipimo vipya ili waweze kuacha na ulimaji usio kuwa na tija.
0 Comments