Na Gabriel Kilamlya NJOMBE
Wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA Wilaya ya Njombe wameonywa juu ya kuchelewesha ujenzi wa miradi mbalimbali ya miundombinu ya barabara na madaraja zikiwemo barabara za kiwango cha lami nyepesi za Nazareth na Lutilage mjini Njombe.
Onyo hilo limetolewa na Kamanda wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Mkoa wa Njombe Cassim Ephraim wakati akitoa ripoti ya utendaji kazi ya kipindi cha miezi mitatu ambapo amesema kusuasua kwa miradi hiyo kuna tia shaka namna walivyowapata makandarasi wa kutekeleza miradi hiyo.
Kamanda Cassim amewataka wananchi pia kutoa taarifa haraka pindi wanapokuta miradi mbalimbali ikisua sua katika maeneo yao na kwamba hii itasaidia kuharakisha ujenzi huo.
Aidha kamanda huyo amesema katika kipindi hicho cha miezi mitatu pia wamefuatilia ujenzi wa daraja la Mabatini linalovusha watu toka Njombe mjini kwenda Ramadhani na kubaini baadhi ya kasoro.
Kituo hiki kimefanya mazungumzo na baadhi ya wakazi wa mtaa wa Nazareth mjini Njombe ambao ni wanufaika na barabara hiyo akiwemo Riziki Kilumile na Benson Msigwa Wanasema barabara hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikijengwa taratibu sana jambo linalowapa wakati mgumu katika kuitumia.
Pamoja na mambo mengine Takukuru imesema inaendelea kupokea taarifa mbalimbali zinazohusiana na vitendo vya Rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na ofisi.
0 Comments