Header Ads Widget

MBUNGE WA JIMBO LA MOSHI VIJIJINI PROF PATRICK NDAKIDEMI AENDELEA NA ZIARA KWA KUTEMBELEA KATA YA KIMOCHI.

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI.

Mbunge wa jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata ya Kimochi na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi hao.


Aidha Mbunge huyo alitumia pia nafasi hiyo kuwahamasisha wananchi kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la Sensa litakalofanyika Agosti 23 mwaka huu.




Mbunge huyo aliyeongozana na Diwani wa Kata hiyo, Ali Badi, viongozi wa serikali na chama katika ngazi ya vijiji na kata, wataalamu kutoka TARURA, MUWSA na TANESCO.


Akihutubia wananchi  katika vijiji vya Sango na Mowo, wananchi walieleza kero ya kuchelewa kupatikana maji safi na salama pamoja na kwamba Serikali imeshapeleka kiasi cha milioni 500 kutatua kero hiyo.



Wananchi hao pia walikerwa na kitendo cha baadhi ya watu wanaoishi ukanda wa juu kuhofia bomba za mradi kupita kwenye mashamba yao na kuomba mkuu wa mkoa aliyeteuliwa hivi karibuni, Nurdin Babu asimamie kero hiyo ili wananchi wa ukanda wa chini wapate maji. 


Akijibu hoja hiyo, Mbunge Prof. Ndakidemi aliwahakikishia wananchi kuwa mkuu wa wilaya ya Moshi Abas Kayanga ameshatatua kero hiyo, na mradi unatekelezwa kupitia MUWSA. 



Aidha wananchi walimweleza Mbunge kuwa barabara ya Sango hadi Mowo ni mbovu na wakati wa mvua kuna changamoto ya kutokupitika kabisa kutokana na utelezi na kuomba ukarabati ufanyike kwa kiwango cha lami.


 Mbunge na wataalamu wa TARURA walieleza kuwa wameibeba kero hiyo na watashauri ukarabati ufanyike kwa kiwango cha moram au changarawe. 


Prof. Ndakidemi alikagua mradi wa ujenzi wa ofisi ya kijiji cha Sango unaoendelea kwa nguvu za wananchi ambayo imefika hatua ya boma na kumpongeza Diwani wa Kata hiyo, wananchi na wadau wa maendeleo kwa kuchangia na kujenga ofisi ya kijiji Chao.


Akiwa katika kijiji cha Mowo, Mbunge aliwaambia wananchi kuwa anakerwa na tabia inayojitokeza ya kupinga miradi ya maendeleo katika vijiji vya Lyakombila na Mowo. 


"Nilipokuja hapa nimeambiwa kuna baadhi yenu wanapinga mradi wa maji unaotekelezwa na MUWSA kwa gharama ya shilingi milioni 500 niwaase wanakijiji kuweni makini na watu wa namna hiyo kwani hawaitakii  kata ya Kimochi mambo mema" alisema Prof. Ndakidemi.


Alisema kuwa, wakati wa kampeni wananchi walielezea kero ya maji na amepambana Serikali imetoa fedha ya kutatua changamoto hiyo ya maji lakini kwa sasa wananchi wanawageuzia kibao hivyo wao kama viongozi hawawaelewi.


"Nakumbuka mlikuwa mkilalamikia tatizo la maji sasa tumepambana mpaka Serikali imetupa fedha ya kutatua changamoto ya maji mnatugeuzia kibao wananchi sisi viongozi hatuwaelewi" Alilalamika Mbunge Prof. Ndakidemi.

 
Mbunge huyo na Diwani waliwahakikishia wananchi wa Kata ya Kimochi kwamba wao kama viongozi hawatakatishwa tamaa na wapinga maendeleo na wataendelea kutekeleza kwa matendo ilani ya Chama cha Mapinduzi.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI