NA HADIJA OMARY, MATUKIO DAIMAAPP
LINDI
Ikiwa siku ya kesho Augost 23 /2022 ndio zoezi la Sensa likitarajiwa kufanyika Wananchi wa Mkoa wa Lindi wametakiwa kujitokeza kuhakikisha kila mmoja anaingia kwenye orodha ya kuhesabiwa ili kuifanya Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa usahihi katika Sekta mbali mbali ikiwemo Afya
Wito huo umetolewa na Mbunge wa jimbo la Lindi Hamida Abdallah leo alipokuwa anazungumza na wananchi wa jimbo hilo katika Mkutano wa hadhara wenye lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi la Sensa linalotarajia kufanyika hapo kesho uliofanyika katika viwanja vya Mtaa wa Kongo Manispaa ya Lindi Mkoani humo
Hamida alisema pamoja na kwamba Serikali imewekeza vya kutosha katika Sekta ya Afya ili kupunguza vifo vya akina Mama wajawazito na Watoto wachanga bado kuna changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hiyo ya Afya ikiwemo upatikanaji wa dawa.
Alisema changamoto hiyo ya ukosefu wa dawa inatokana na idadi ndogo ya watu ambayo ilikuwa inaonyesha katika maeneo hayo kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya watu na makazi iliyofanyika katika mwaka 2012.
"Sasa ndugu zangu wananchi wa Lindi mjini hii ni fulsa kubwa kwetu kuhakikisha kwamba siku ya kesho tarehe 23 tunajitokeza kila mmoja wetu kuhakikisha anashiriki katika kujiandikisha ili tusirudie makosa yale ya miaka iliyopita "
"Sensa hii ni fursa sana kwetu kwani sensa ya mwaka 2012 sisi wanachi wa Lindi mjini tuliathirika sana wananchi wengi hawakujitokeza kuhesabiwa kwa sababu mbali mbali watu wasiyo itakia mema Nchi yetu walikuja wakatudanganya na sisi tukawasikiliza" alisema Hamida
Kwa upande wake Aisha Amiri Mkazi wa kata ya Mitandi alisema kuwa changamoto ambazo zitajitokeza endapo watu hawatahesabiwa hesabiwa Serikali itakosa Takwimu sahihi zitakazoiwezesha kutoa huduma kwa wananchi wake kama inavyotarajiwa.
" kwa mfano tukihesabiwa na kupata takwimu sahihi maana yake hata ile Ruzuku inayotoka Serikali kwa ajili ya akina Mama wajawazito na Watoto wachanga itakuwa haitoshelezi mahitaji" alisema Bi Aisha.
Nae Rukia Selemani Mkazi wa Manispaa ya Lindi alisema kuwa changamoto nyingine iliyopo kwa sasa inayowakuta akina mama wengi wanaokwenda kujifungua ni kutakiwa kulipa gharama za matibabu licha ya Serikali kupitia Sera ya Afya kueleza kuwa huduma za Afya kwa akina mama wajawazito kuwa ni bure.
" kwa miaka ya nyuma Sera hii ilikuwa inatekelezeka lakini kwa miaka ya hivi karibuni hili limebaki kwenye makaratasi tuu Mfano mama akiwa mjamzito na kutakiwa kufanyiwa upasuaji atalazimika kulipia kiasi cha pesa ili aweze kupata huduma pengine hili la matibabu bure linashindwa kutekelezwa kutokana na Wingi wa akina mama wanaokwenda kujifungua"
"Lakini yote kwa yote kama hiyo ni kweli basi wananchi hatuna budi kushiriki katika zoezi hilo la Sensa ikiwa pamoja na kutoa taarifa za kweli na za usahihi ili kuiwezesha Serikali kupata Takwimu zitakazo tusaidia kumaliza changamoto hizo" alimaliza Bi. Rukia
0 Comments