NA WILLIUM PAUL, MATUKIODAIMAAPP,MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Vunjo Dkt. Charles Kimei ametembelea Kata ya Mwika Kaskazini na kujionea ujenzi wa Kituo cha Polisi kinachojengwa kwa nguvu za wananchi.
Mbunge huyo ameridhishwa na jitihada zilizofanywa na wananchi na kutoa ahadi ya kuchangia kiasi cha shillingi Milioni 3 ili kuendelea kukamilisha hatua ya upauaji wake.
Aidha, Mbunge aliweza kusikiliza kero mbalimbali za wananchi ambapo kero kubwa ni ukosefu wa Maji Safi na salama kwa maeneo mengi Kata ya Mwika Kaskazini na kuwaeleza jitihada anazozifanya kwa Waziri wa Maji ili kuhakikisha Mradi unapata Fedha kwa wakati kusaidia kukamilika kwake.
Kwa upande wa MUWSA ambao wanahudumia huduma ya Maji Kata ya Mwika Kaskazini wameeleza changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha kuwezesha kukamilisha Mradi wa Maji na kutumia nafasi hiyo kumshukuru Mbunge kwa kuendelea kuwatetea wananchi kupata Fedha za Mradi kwa wakati ili kero ya Maji itatuliwe kwa wakati.
Dkt. Kimei amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaunga mkono wananchi wa Jimbo la Vunjo kuleta Maendeleo mbalimbali kupitia Bajeti ya Serikali.
Pia, Mbunge aliendelea kuhamasisha wananchi wote wa Jimbo la Vunjo kujiandaa na zoezi la Sensa na Makazi ya watu Agosti 23 mwaka huu na kuwaeleza wananchi watoe taarifa sahihi ambazo zitatumika katika kupanga Mipango yote ya maendeleo.
Katika ziara hiyo Dkt. Kimei aliongozana na Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Kilimanjaro Esther Maleko ambapo alimpongeza Mbunge Dkt. Kimei kwa kazi nzuri anayoifanya katika Jimbo la Vunjo.
Esther alihamasisha vikundi kujisajili na kuomba mikopo ya Halmashauri ya asilimia kumi ambapo pia alizungumzia swala la ukatili wa kijinsia kuhamasisha jamii kuacha tabia ya kuwalinda wahalifu wanaotenda ukatili huo kwa watoto na badala yake watoe ushirikiano kwa vyombo vya Usalama ili haki iweze kutendeka.
Kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Mwika Kaskazini, Diwani Samwel Shao amemshukuru Mbunge Dkt. Kimei kwa kuendelea kuwasemea katika miradi mbalimbali ya maendeleo na kumuahidi kuendelea kutoa ushirikiano.
0 Comments