NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, Ramadhani Mahanyu amesema kuwa zoezi la Sensa la mwaka huu ni la mfano wake kwani mwananchi unatoa taarifa kwa uwazi.
Mahanyu ametoa kauli hiyo mara baada ya kuhesabiwa na karani wa sensa ambapo alisema kuwa, sensa inaisaidia Serikali kujua idadi ya wananchi wake na kupanga bajeti kulingana na watu waliopo.
"Sensa inasaidia wananchi kuleta maendeleo kwani Serikali itagawa maendeleo katika maeneo mbalimbali kulingana na idadi ya watu waliopo hivyo niwaombe wananchi kujitokeza kwa wiki kuhesabiwa" alisema Katibu Mahanyu.
Alisema kuwa, makarani na wasimamizi wa sensa wamekuwa wakiendesha zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa na kuwaomba wananchi kuwaunga mkono kwa kuwapa taarifa sahihi.
Katibu huyo aliwataka wananchi ambao hawatafikiwa leo na makarani hao wa sensa kuwa na amani kwani zoezi hilo linaendeshwa kwa siku saba hivyo watafikiwa kila mmoja.
Alisema kuwa, zoezi la Sensa kwa wilaya ya Moshi vijijini kichama linaendelea vizuri na hakuna malalamiko yoyote ambayo yamemfikia na kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano.
Katika hatua nyingine, Mahanyu alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hasani kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo makubwa.
"Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2022/2023 imemgusa kila mwananchi katika sekta mbalimbali na hii inajidhihirisha kuwa imedhamiria kuwatumikia wananchi kwa dhati kubwa" alisema Mahanyu.
Mwisho.
0 Comments