Leo Jumamosi Agosti 6, 2022 Tanzania inatupa karata zake nne za mwisho katika Michezo ya 22 ya Jumuiya ya Madola inayoendelea jijini Birmingham, Uingereza, wakati mabondia wake Wawili na wanariadha idadi hiyo hiyo wakiingia dimbani kupambania medali.
Kwa upande wa ndondi bondia Yusuf Lucasi Changalawe atapambana na Sean Lazzerini wa Scotland katika nusu finali ya kwanza ya uzani wa 75kg-80kg (Light Heavyweight ) katika Ukumbi Namba 4 wa National Exhibition Centre (NEC) majira ya saa 6:30 mchana kwa saa za Uingereza ama saa 8:30 mchana kwa saa za Tanzania.
Karata ya pili ya Tanzania itatupwa katika ndondi tena wakati bondia Kassim Selemani Mbundwike atakapopambana na Tiago Osorio Muxanga wq Msumbiji katika nusu finali ya pili ya uzani wa 67kg-71kg (Light Middle) katika Ukumbi huo huo wa NEC majira ya saa 10:45 za jioni saa za Uingereza ama saa 12:45 za jioni kwa saa za Tanzania.
Mshindi katika mapambano hayo mawili ya ndondi atatoa matumaini kwa Tanzania kupata medali ya Dhahabu ama ya Fedha, kulingana na matokeo ya mchezo wa fainali utakaocheza siku ya Jumapili, ambapo mshindi atabeba Dhahabu na wa pili ni Fedha.
Ikumbukwe kwamba hadi kufikia wakati huu wa Changalawe na Mbundwike kucheza hatua hiyo ya nusu finali leo kila mmoja wao tayari ana medali ya Shaba, kwani katika ndondi mabondia wote wanaofika hatua hiyo huwa moja kwa moja wanatunukiwa medali hiyo, hata kama watashindwa katika mchezao wao wa nusu fainali.
Karata zingine mbili zilizosalia wanazo wanariadha Josephat Joshua Gisemo na mwenzie Faraja Lazaro Damasi ambao watakuwa bega kwa bega katika dimba moja katika fainali ya mbio za mita 5,000 Uwanja wa Alexander mnamo majira ya saa 2:10 jioni kwa saa za Uingereza ama saa 4:10 Usiku kwa saa za Tanzania.
Gisemo na Damasi ni miongoni mwa wanariadha 20 kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola watakaowania medali za Dhahabu, Fedha na Shaba.
0 Comments