Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Hali ya Hawa Hussein Mwenye umri wa Miaka 26, mwanamke aliyejeruhiwa kwa kumwagiwa maji ya moto katika Manispaa ya Shinyanga inaendelea vizuri kutokana na matibabu anayopatiwa katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Matukio Daima leo imefika tena katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ili kumjulia hali majeruhi huyo, ambaye hali yake imeendelea kuimarika kutokana na huduma za matibabu anazoendelea kupatiwa.
Akizungumzia hali ya majeruhi huyo Mganga mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Luzila John amesema hali ya mama huyo imeendelea kuimarika ikilinganishwa na siku aliyofikishwa katika Hospitali hiyo.
Dkt. Luzila kuwa mama huyo alifika katika Hospitali hiyo akiwa amejeruhiwa kwa kuunguzwa na maji ya moto sehemu ya kifuani, Tumboni, Mikononi pamoja na mapajani.
''Tulipata mgonjwa anaitwa Hawa Husein ambaye alikuwa amejeruhiwa kwa maji ya moto alikuwa ameungua sehemu za kifua chake, alikuwa ameungua pia kwenye mapaja baada ya kumuona kiwango cha kuungua eneo zima alilokuwa ameungua ni asilimia 12 kwahiyo tukampa huduma zake za awali lakini pia tulimpa dawa kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya Bakteria kwenye ngozi maendeleo yake ni mazuri akiwa anaendelea na hizo dawa za kupaka pamoja na zakumeza tunategemea kabla ya wiki hii kuisha atakuwa amepata maendeleo mazuri na tutakuwa tunaweza kumruhusu. amesema Dkt Luzila
Agasti Mosi Mwaka huu majira ya saa tatu usiku mwanamke anayeitwa Hawa Hussein mkazi wa kata ya Kambarage katika Manispaa ya Shinyanga alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kumwagiwa maji ya moto na jirani yake aliyetajwa kwa jina la Goergia Juli.
Hata hivyo juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Matukio Daima ili kujua hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo, ambapo mpaka sasa jeshi la polisi halijatoa taarifa yoyote kuhusu tukio hilo.
0 Comments