Header Ads Widget

WANANCHI KIJIJI CHA KITOMONDO WATOA MALALAMIKO KWA MBUNGE

 


WANANCHI wa Kijiji cha Kitomondo Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wametoa malalamiko kwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo kupigwa kwa kudaiwa kuingia kwenye eneo la mwekezaji.


Wakizungumza kwenye kikao cha Kijiji hicho walisema kuwa wamekuwa wakipigwa na walinzi kwenye eneo hilo wanapoingia kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo na kuokota kuni pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu.


Kaimu mtendaji wa Kijiji hicho Makoye Kayungilo alisema kuwa eneo hilo licha ya kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha lakini uongozi wa Kijiji cha Mafizi unasema kuwa Kijiji hicho kiko Halmashauri ya Kisarawe.


Moja ya wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Michael Kilila alisema kuwa alikamatwa na mgambo na kupigwa hadi kuumizwa mkono na kupelekwa Kijiji cha Mafizi na kupigwa faini ya shilingi 600,000.


Kilila alisema kuwa alifuatwa kwa mara nyingine tena ambapo alipelekwa Polisi na baadaye aliambiwa akihitajiwa ataitwa tena hali ambayo inawafanya wasiishi kwa amani. 


Kidawa Shaban alisema wao walikuwa wamekwenda kwenye eneo hilo kukata kuni lakini walikamatwa na baadaye Polisi waliwachukua na kuwapeleka Polisi na baadaye waliachiwa.


Akijibu hoja hizo Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo alisema kuwa suala hilo atalipeleka kwa mkuu wa mkoa kwani linahusisha Wilaya mbili ili lipatiwe ufumbuzi.


Mwakamo alisema kuwa mara baada ya kulipeleka suala la mgogoro huo wanapaswa kutoa ushirikiano na wasiseme uongo pale watakapotakiwa kutoa maelezo ili ukweli uweze kupatikana.


Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo alisema kuwa hajapokea taarifa ya matukio hayo ya kupigwa wananchi lakini atalifuatilia ili kujua wahusika ili hatua zichukuliwe.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI