Katibu Mkuu, ACT Wazalendo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Julai 7, 2022 jijini Dar es Salaam.
NA ARODIA PETER, MATUKIODAIMAAPP,
Chama cha ACT Wazalendo kimesema wananchi hawaridhishwi na kasi ya Serikali katika kushughulikia hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili kwa sasa.
Kimesema kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu za chakula, mafuta ya petroli, dizeli na vifaa vya ujenzi kumechangia kupanda kwa gharama za maisha na hali ngumu ya uchumi kwa wananchi hasa wa hali ya chini.
Kimesema kupanda kwa petroli na dizeli ndiko kunachochea kwa sehemu kubwa kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu na nauli.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Julai 7, 2022, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu Ado alisema bei za bidhaa muhimu kama mchele, unga wa mahindi, mafuta ya kupikia na maharagwe zimepanda sana ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana.
Ado alisema ugumu huo wa maisha kwa wananchi wameubaini kupitia ziara ya Sekretarieti ya chama hicho Taifa katika kata zote 10 za Jimbo la Mbagala Dar es Salaam kuanzia Juni 26 hadi Julai 6 mwaka huu ikiongozwa na yeye mwenyewe katibu mkuu.
"Katika ziara hiyo tumetembelea maeneo ya masoko, vijiwe vya kahawa, bodaboda na kufanya mazungumzo na wazee, tumebaini mchele umepanda kutoka Sh 1200 hadi 2400, unga wa mahindi umepanda kutoka Sh 1000 hadi Sh 1600, mafuta ya kupikia kutoka Sh 3000 kwa lita hadi Sh 9000.
Bidhaa nyingine ni unga wa ngano umepanda kutoka Sh 1200 hadi Sh 2000, sukari kutoka Sh 1500 hadi Sh 3000 huku nyama ikipanda kutoka Sh 6500 hadi Sh 9000." alisema Ado.
Kufuatia hali hiyo ACT Wazalendo kimerejea kwenye ushauri wake kilioutoa siku chache zilizopita kwamba Serikali iondoshe Sh 500 kwa kila lita ya mafuta ya dizeli na petroli zinazokusanywa kama tozo ambapo itakuwa imeweka ruzuku ya Sh bilioni 152.5 kila mwezi badala ya Sh bilioni 100.
Aidha chama hicho kimesisitiza umuhimu wa Serikali kuingilia kati kwa kuyawezesha mashirika ya Maendeleo ya Petroli nchini (TIPPER) na TPDC kuagiza mafuta ili kuhakikisha unafuu zaidi unapatikana sambamba na kutenga fedha haraka kwa ajili ya kuongeza uwezo wa hifadhi ya mafuta ya petroli ili kuongeza siku zaidi tofauti na utaratibu wa sasa wa kuagiza kila mwezi.
0 Comments