NA BERDINA MAJINGE NA ZUHURA ZUKHERI
MATUKIO DAIMA APP.
Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Iringa kimepokea kwa masikitiko makubwa kwa kadhia ya janga la moto, pamoja na athari zilizotokea huku wafanya biashara wengi wakiathirika kwa kupata hasara kwa kuunguliwa na bidhaa zao.
Akizungumza mbele ya mamia ya wafanyabiashara waliokusanyika katika Soko la Mashine Tatu lililoungua mjini Iringa,Mjumbe wa Kamati kuu ya chama cha mapinduzi Taifa salim Abri Asas alisema kuwa wapo waliochukua mikopo kwa ajili ya kuendesha biashara zao na wanatakiwa kuzirejesha kutokana na mauzo.
MCC Asas alisema kuwa anawapa pole Baraza kuu la waislam Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Iringa ambao ndio wamiliki wa eneo hilo ambao nao wamepata hasara kwa kuunguliwa na maeneo yao.
"Tumeumia, CCM ipo pamoja nanyi niwahakikishie hatuwezi kuwageuzia mgongo,tunasubiri tathmini na tutasaidia hapa na pale mrejee katika shughuli zenu,na kama wahusika wa soko hili wakihitaji msaada wa kuboresha miundombinu, tutashiriki bila kusita."
Asas alikiri kwa masikitiko makubwa kwamba janga la moto lililoteketeza zaidi ya biashara 500 limeacha maumivu makubwa kwa wafanyabiashara wengi wa kipato cha chini, hasa wale waliokuwa wamechukua mikopo ya kujikimu kimaisha.
Asas amewahakikishia wahanga kuwa CCM iko nao bega kwa bega, na itahakikisha misaada, michango, na jitihada za kuwainua zinapangwa kwa utaratibu mzuri.
Alisema kuwa chama cha mapinduzi ilipendekeza na kufatilia kwa ukaribu kuhusu eneo maalum la wafanyabiashara wadogo na kuamua kuwa stendi ya daladala iliyopo katikati ya mji huo kujengwa jengo kubwa la kisasa la Machinga Complex ambapo wafanyabahara wote watafanyia biashara zao katika jengo hilo.
"Kwanini stendi ya daladala isitumike kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, kwa kujengewa Machinga Complex ambapo wafanyabiashara wadogo na Machinga wote watafanya biashara hapo? ambapo Ombi hilo limekubaliwa na lipo katika hatua ya mchoro kwa ajili ya kujenga na daladala itafutiwe eneo lingine"alisema
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Iringa Benjamin Sitta amelitaka baraza kuu la waislam Tanzania kuanza utaratibu haraka wa kurudisha eneo la biashara la mashine tatu ikiwa ni Pamoja na kuweka miundumbinu mizuri ya soko ili kukabiliana na majanga pindi yanapotokea.
DC Sitta alisema kuwa eneo hilo la soko lipo chini ya Bakwata hivyo serikali haina mamlaka ya kisheria bali hushauriana ili kuhakikisha wafanyabiashara wanarudi katika maeneo yao.
Aidha mkuu wa wilaya ya Iringa Sitta ameiomba bakwata kuhakikisha utaratibu huo unakuwa na mpangilio mzuri wa vyumba vya biashara ili iwe rahisi kukabiliana na changamoto mbalimbali zinapojitokeza.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru sana Bakwata lakini niwaombe muhakikishe mnafanya utaratibu wa haraka kuhakikisha wafanyabiashara wanarudi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi, lakini niwaombe ndugu zangu wa Bakwata hakikisheni mnapoanza utaratibu mpangilio unakua mzuri wakuwezesha kufanya uokoaji katika majanga mbalimbali, leo hii eneo hili lingekuwa na mpangilio mzuri wakuwezesha njia za kupita hili tatizo lingeweza kudhibitiwa mapema na madhara yasingekuwa makubwa kama haya” alisema DC Sitta.
Akizungumzia wafanyabiashara wenye mikopo ya kausha damu DC Sitta amewataka wote watakaosumbuliwa na wakopeshaji wafike ofisini kwake mapema kutoa taarifa ili waone jinsi ya kushughulikia tatizo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Baraza kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Iringa Kabigili Said amesema kuwa watajitahidi kufanya marekebisho ya miundo mbinu haraka iwezekanavyo ili wafanya biashara waweze kurejea katika maeneo yao.
"Tutajitahidi kurekebisha miundo mbinu ya soko hilo kwa sababu wafanyabiashara wengi wanaendesha biashara zao kwa mikopo ili waweze kurudi katika hali yao nzuri ya kiuchumi na kuweza kufanya marejesho"alisema
Naye Mwenyekiti wa soko la mashine tatu Jafari Maulid alisema kuwa wameathirika kibiashara kutokana na moto kuteketeza kila kitu katika eneo hilo hivyo anaiomba serikali kupitia mkuu wa wilaya kuwasaidia kuweka utaratibu utakao wasaidia wafanyabiashara waliokopa mikopo binafsi kutosumbuliwa kwani hakuna mfanyabishara aliyetoka na kitu katika eneo hilo.
Aidha mwenyekiti huyo ameiomba serikali kuweka ulinzi katika mali zilizosalia kama vile ukusanyaji wa mamabati chakavu.
MWISHO.
0 Comments