NA HAMIDA RAMADHAN DODOMA
RAIS Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri Mkuu na Mkuu wa wa mkoa wa Dodoma kutenga eneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa mnara wa mashujaa utakaoendana na hadhi ya Makao makuu ya nchi.
Licha ya ujenzi wa mnara kuwa na hadhi ya Makao makuu, Rais Samia ametaka kutekeleza Mradi huo kwa gharama nafuu.
Samia aliyasema hayo leo Jijini hapa wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya sherehe za Mashujaa ambazo kitaifa zilifanyika Jijini Dodoma.
Alisema Jiji la Dodoma linakuwa kwa kasi na uwanja huo wa Mashujaa upo katikati ya mji aliagiza mnara huo uhamishwe na kujengwa sehemu nyingine kwenye eneo kubwa kwa gharama za fedha zitakazo stahamilika.
"Naomba nipendekeze kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi na Mkuu wa mkoa wa Dodoma tafuteni eneo kubwa na bora zaidi kujenga mnara wenye hadhi ya makao Makuu kwa gharama nafuu," alisema Rais Samia
Aidha aliagiza Ofisi ya Waziri Mkuu na vyombo vya Ulinzi na usalama kuja na utaratibu wa maadhimisho ya siku hiyo wenye gharama nafuu.
Akizungumzia umuhimu wa siku hiyo Rais Samia alisema Viongozi na Wananchi wa kila Mkoa wanashiriki siku hiyo kwa kufika kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuadhimisha siku hiyo.
"Niwashukuru wote walioshiriki katika maandalizi na maadhimisho haya kokote walipo nchini Tanzania kwani Mashujaa waliopigania Uhuru walipambana katika nyanja mbalimbali dhidi ya ukoloni, udhalimu,ubeberu na ukandamizaji na walipambana kifikra na kwa vitendo," alisema.
Alieleza kuwa katika vita walivyopambana mashujaa hao ni pamoja na vita vya majimaji na vita vya pili vya dunia ambavyo uwepo wa wazee waliombatana ni uthibitisho tosha walikuwepo katika mapigano hayo.
Kadhalika alisema Mashujaa hao walipambana kwenye vita vya Mapinduzi ya Zanzibar, Vita ya ukombozi wa Afrika hasa Afrika Kusini, Vita vya Kagera na katika Oparesheni mbalimbali ndani na nje ya Afrika .
" Leo tuko hapa tunakumbuka na kuwaenzi mashujaa hawa waliojitoa mhanga kwa kutetea na kulinda Uhuru wa uhai wetu na heshima ya Bara la Afrika na Sherehe hizi zitaendelea kila mwaka ,
"Maadhimisho hayo sio tu kwa waliopoteza maisha yao tu bali hata wale waliopata Ulemavu wa maisha na waliotoa michango ya mbalimbali ya aina moja au nyingine," aliongeza
Aidha Rais Samia alisema Taifa la Tanzania haliwezi kusahau mchango mkubwa wa uhai,mali na hali uliofanywa na Mashujaa na kwasababu hiyo kila mwaka inaadhimishwa siku hiyo ya kumbukumbu.
Sambamba na hilo alibainisha kuwa siku hiyo inaadhimishwa kwa kuwakumbuka waasisi wa Taifa ambao pia ni Mashujaa waliotangulia mbele za haki.
"Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Shekhe Abedi Amani Karume na wengine walioshirikiana nao au waliokuja baada yao kuendeleza aliyoyaanzisha kwani mchango wao mkubwa ndio unaoifanya Tanzania kuwa nchi ya amani na yenye kufuata misingi ya haki na utawala bora.
Alisema misingi na tunu walioiacha nchini ndio imeifanya Taifa kutambulika Kimataifa.
Alisema kwakutambua kazi ya ukombozi iliyofanywa na mashujaa hao hakuna budi kuendelea kuwaenzi kwa kudumisha amani, upendo na mshikano.
Aidha alisema ushujaa sio kupambmba katika vita bali hata kuweka nchi salama kwa kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa usalama wa chakula, maji safi na salama.
Aidha alisema wananchi wanahitaji huduma bora za afya, elimu na uwepo wa umeme kwa ajili ya kujenga uchumi unaoendana ili kutokomeza ujinga na kuwezesha mtu kujikimu.
UGONJWA WA UVIKO 19
Rais Samia aliwataka Wananchi kuendelea kujitokeza na kuchanja chanjo ya UVIKO 19 ili kujikinga na Magonjwa
KUHUSU ZOEZI LA SENSA
Rais Samia aliwataka Wananchi wote ifikapo Agosti 23 kushiriki kikamilifu Katika zoezi la Sensa ya Watu na makazi kwa ajili ya Maendeleo ya Taifa.
Hata hivyo Katika maadhimisho hayo Viongozi mbalimbali wakitaifa na wastaafu wa Tanzania na Zanzibar walishiriki maadhimisho hayo.
Mwisho
0 Comments