*************
Teddy Kilanga,Arusha
Serikali imepunguza wingi wa mifumo ya usajili,malipo ya ada ya leseni na tozo mbalimbali katika sekta ya utalii ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa wadau wa sekta ya utalii uliofanyikia jijini Arusha,Dkt.Chana alisema maamuzi hayo yametokana na maagizo ya Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyekiti wa baraza la Taifa la biashara (TNBC) aliyoyatoa katika mkutano wa 13 wa baraza hilo uliofanyika jijini Dodoma.
"Nataka kutoa mrejesho kwamba wizara ya maliasili na utalii imeanza kulifanyia kazi pendekezo la kutengeneza mfumo wa one stop shop kwa ajili ya ulipaji wa ada,tozo na malipo yote ya ndani ya sekta ya utalii,"alisema Dkt.Chana.
Aidha Waziri Chana ameongeza kuwa wizara inafanya mazungumzo na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa lengo la kutatua changamoto za tozo kwa watalii wanaopita kwenda kwenye maeneo ya utalii wa utamaduni.
Pia alisema wizara ya maliasili na utalii inapitia sheria na kanuni mbalimbali katika sekta hiyo ikiwemo suala la kuboresha mfumo wa ulipaji wa tozo ya maendeleo ya utalii(Tourism Development Levy-TDL)
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii,Prof.Elihamani Sodoyeka alisema sera ya utalii nchini imejikita katika kuendelea katika kuchochea uendelezaji wa utalii kwa lengo la kuongeza wigo wa mazao yatokanayo na utalii ili kufikia adhma ya serikali katika kuhakikisha idadi ya watalii inaongezeka.
Naye Katibu Mtendaji wa baraza la Taifa la biashara,Dkt.Godwil Wanga alisema sekta ya utalii inamchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi kwa hiyo changamoto yoyote inayoweza kurudisha nyuma sekta hiyo itaathiri sana Taifa.
Mshauri wa mazingira ya uwekezaji kutoka shirika la fedha la Kimataifa(IFC) lililo ndani ya benki ya dunia,Anita Kundy alisema mapendekezo hayo yamekuja wakati muhimu sana nchini Tanzania ikiwa ni mafanikio ya uzinduzi wa filamu ya Royal tour katika kutangaza utalii .
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo ambaye ni Mpagazi Olosiyo Mollel waliiomba serikali kurudisha asilimia ya fedha katika hifadhi mbalimbali kwa ajili ya kuboresha miundombinu kwani sasa hivi watalii wanaongezeka zaidi.
0 Comments