AMON MTEGA MADABA.
KUMEKUWEPO na Jitihada mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya tatizo la Ajira hasa kwa Vijana hapa Nchini na kuwafanya baadhi ya Vijana kukata tamaa ya kujishughulisha katika sekta mbalimbali jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya Jamii na Taifa kwa ujumla.
Kufuatia hali hiyo baadhi Viongozi kwa kushirikiana na wamekuwa wakipambana na changamoto hiyo kwa kuweka matamasha mbalimbali ambayo yaliyokuwa yakielekeza namna gani Vijana wanaweza kuzitumia fursa zilizopo kwenye maeneo yao kisha kuzifanyia kazi na mwisho wa siku zinakuwa ni sehemu ya Ajira kwao.
Baadhi ya Viongozi hao ambao wamekuwa mstali wa mbele kukabiliana na changamoto hizo kwa kutoa fursa kwa Vijana ni Mbunge wa Jimbo la Madaba Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Dr.Joseph Kizito Mhagama ambaye amefanya tamasha la kuwainua kiuchumi Vijana wa Jimbo hilo kwa kutumia fursa zinazowazunguka kwenye eneo hilo.
Dr.Mhagama wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa tamasha hilo ambalo limebeba ujumbe mbalimbali kama wa Vijana kutumia vipaji vyao kama sehemu ya fursa pamoja kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupata tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali hapa Nchini kiwemo ya barabara.
Mbunge huyo amesema kuwa mkakati wa kukuza uchumi na kuibua vipaji kwa vijana unalenga kutatua changamoto za ajira zinazowakabili vijana hao ambao baadhi yao wamekuwa wakiishia kukata tamaa ya kujitafutia maendeleo .
Amesema kuwa amechunguza kwa kina katika Jimbo hilo amebaini kuwa vijana wengi wanauwezo wa kufanya kazi za kujipatia maendeleo ila tu wanakosa namna ya kupata mwanga wa elimu ya kutumia fursa zilizopo ambazo zimekuwa zikiwazunguka kwenye maeneo yao.
Amefafanua kuwa baada ya kubaini hilo akaamua kuweka mkakati kwa kushirikiana na taasisi za Halmashauri ya Madaba kubuni tamasha ambalo linaloweza kutoa Elimu ya utumiaji wa fursa mbalimbali kwa vijana ambalo litawafanya vijana kuongeza uelewa juu ya utumiaji wa fursa hizo.
Ikumbukwe kuwa Mbunge huyo kabla ya kugombea ubunge wa Jimbo hilo aliibua zao la Tangawizi kwenye Jimbo hilo na kuwafanya wakazi wa eneo hilo wakiwemo Vijana kunufaika huku wakihesabu kuwa zao hilo ni moja ya zao linalowaongezea uchumi hadi leo.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupata tuzo ya miundombinu ambayo imeiletea heshima Taifa la Tanzania na kuifanya iwe kwenye ramani ya maendeleo .
"Ndungu zangu wa Madaba wenzangu mimi Mbunge wenu ndiye ninayejua kuwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kweli kweli na ndiyo maana kapatiwa tunzo hiyo nawaombeni tumuunge mkono kwa nguvu zetu zote"amesema Mbunge Dr.Joseph Kizito Mhagama.
Akizungumzia baadhi ya kazi zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika Jimbo la Madaba ni kutoa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya- Madaba kutoa fedha za kuboresha vituo vya Afya na Zahanati , Ujenzi madarasa Uviko 19 pamoja na mpango wa ujenzi wa barabara ya kiwango lami Mkiu ,Liganga na Madaba ambayo itakuwa ni barabara ambayo itaondoa changamoto kwa wakazi wa Ludewa na Ruvuma kutokana na umuhimu wake.
Aidha amezungumzia barabara nyingine kuwa ni ya Makambako -Songea ambayo ipo kwenye mpango wa kufumuliwa na kuwekewa lami mpya kwa viwango ubora na itaanzia Songea jambo ambalo amesema ni matunda ya Serikali ya awamu ya sita inayoongonzwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Awali akisoma tamko la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan Solana Zenda amesema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto ndogondogo Vijana wanatambua kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuwa wataendelea kumuunga mkono.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema wakati akizindua tamasha hilo kwaniaba ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi ya maendeleo hivyo Wananchi wanatakiwa kuendelea kuiamini.
Naye mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho amesema kuwa chama kinaipongeza Serikali pamoja na Mbunge wa Jimbo la Madaba kwa kusimamia ilani ya chama hicho na kuwafanya Wananchi waweze kuwa na maendeleo ikiwemo kutekeleza miradi mbalimbali ambayo ilikuwa kero kwa Wananchi hao.
Katika tamasha hilo ambalo limehudhuliwa na taasisi mbalimbali ikiwemo ya Wakala wa huduma za Misitu Tanzania Wino ambapo mhifadhi mkuu wa shamba la miti Wino Glory Kasmir amesema Vijana wanatakiwa kuunda vikundi ili waweze kupatiwa miti ya kupanda ikiwemo na fedha za kuhudumia mashamba hayo.
0 Comments