Na Matukio Daima APP,Dar es Salaam
SERIKALI imetoa wito kwa Taasisi zisizokuwa za kiserikali ambazo
zinajihusisha na malezi ya watoto waishio kwenye mazingira magumu
kuwajengea uwezo maafisa ustawi wa jamii ili waweze kutekeleza vyema
majukumu yao yakiwamo kulea watoto ambao hawana wazazi.
Wito huo ulitolewa leo Juni 8 mwaka 2022 na mwakilishi wa Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Hadija Kissa alipokuwa akifungua mafunzo kwa
maafisa ustawi wa jamii waliopo kwenye mradi wa kuwarejesha kwenye
familia zao watoto wanaolelewa na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya SOS Village Tanzania.
Hadija alisema mradi huo wa SOS umekuja wakati muafaka kwani utasaidia
watoto ambao walikuwa wakiishi mbali na familia zao za asili kupata
ndugu zao.
Hata hivyo aliitaka SOS kuhakikisha wanatatua na kuainisha changamoto
zilizofanya watoto kama hao kuzikimbia familia zao.
“Niwapongeze SOS kwa kazi hii nzuri, lakini nitoe wito kwao
wahakikishe zile changamoto zilizowatoa hao watoto kwenye familia zao
zinabainishwa ili ziweze kupatiwa ufumbuzi. Wote tunajua kwamba moja
ya changamoto za watoto kama hao kukimbia familia au makazi yao ya
asili ni pamoja kufanyiwa ukatili, kukosa chakula na mambo mengine
kama hayo”alisema Hadija.
“Niwapongeze zaidi SOS kwa juhudi hizi, mpango huu ninaouzindua leo
umekuja wakati muafaka kwani utapunguza watoto wengi kulelewa mbali na
familia zao lakini pia Serikali kuona ni wapi iweke nguvu kukabiliana
na suala la watoto wa mitaani”alisema Hadija.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mratibu wa Malezi mbadala wa SOS
Tanzania, Onesmo Itozya alisema mradi huo niwa miaka mitatu na unahusu
watoto wenye umri chini ya miaka sita.
Alisema watoto waliopo kwenye mpango huo wa kurejeshwa kwenye familia
zao ni 272 hadi kufikia mwaka 2024 na utahusishwa wale waliokuwa
wanalelewa kwenye vituo vya SOS kutoka mikoa mbalimbali Tanzania bara
na Zanzibar.
Itozya alisema kabla ya kuanza mpango huo, SOS ilifanya tafiti
mbalimbali kubaini changamoto na chanzo cha watoto hao kutoka makwao
na kuzifanyia kazi ili zisije kujirudia.
“Tunataka watoto hawa ambao tumekuwa nao kwenye makao ya SOS kwa
kipindi kirefu, wengine tumekaa nao kwa zaidi ya miaka 10 tuwarejeshe
kwenye familia zao ili waendelee kufurahia maisha wakiwa kwenye
tamaduni zao, koo zao, wajomba, mashangazi mababu kama walivyo watoto
wa familia zingine.
“Katika utafiti wetu tumegundua baadhi ya watoto hatuna ulazima wa
kuendelea kukaa nao kwani wana ndugu zao wa damu, hivyo
tunawaunganisha nao ili waweze kuendelea na maisha ya familia zao
halisi.
Hata hivyo, Mratibu huyo wa SOS alisema wale ambao wamebainika hawana
makawao au ndugu zao hawakubainika wakishavuka umri wa miaka sita
watapatiwa makazi mengine mbadala.
0 Comments