MBUNGE wa Jimbo la Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro Prof. Patrick Ndakidemi amesema kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 imejikita katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Prof. Ndakidemi ametoa kauli hiyo leo alipozungumza na kituo kimoja cha Radio ambapo alisema kuwa yapo mambo ambayo Wabunge walikuwa wakiyapigia kelele Bungeni lakini bajeti hiyo imekuja na majibu.
Alisema kuwa miongoni mwa mambo ambayo amekuwa akiyapigia kelele yeye ni upatikanaji wa hospitali ya wilaya katika Jimbo hilo ambapo kwa sasa wameshapata fedha za awali milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya katika Kata ya Mabogini.
Akijibu swali la baadhi ya halmashauri nchini kupata hati chafu katika ripoti ya Mkaguzi wa hesabu za Serikali Mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Mkuu wa wilaya, watumishi wa Halmashauri pamoja na Madiwani kwa kupata hati safi kwa miaka sita mfululizo.
"Nishukuru Halmashauri yangu ya Moshi imepata hati safi kwa miaka sita mfululizo niwapongeze mkurugenzi na Mkuu wa wilaya pamoja na watumishi wa Halmashauri lakini katika zile halmashauri ambazo zimepata hati chafu Waziri wa fedha alishaagiza wale wote waliochangia kupata hati chafu washughulikiwe.
Akizungumzia swala la zao la kahawa Mbunge huyo alisema kuwa zao hilo limekuwa likitoa mchango mkubwa katika kukuza pato la Taifa japo kwa sasa limeshuka lakini bado ni zao la pili linaloingia Serikali fedha za kigeni likizidiwa na Korosho.
Aliongeza kuwa, Serikali ikiboresha baadhi ya vitu kwa kushirikiana na Tacri kuzalisha miche bora zao hilo litaendelea kukua na kukuza pato la Taifa na kwa wakulima wenyewe.
"Uwezekano wa kahawa kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa ni mkubwa japo kwa sasa limeshuka lakini bado ni zao la pili linaloingia Serikali pato la kigeni lakini Serikali ikiboresha zaidi zao hili litaendekea kukua" alisema Prof. Ndakidemi.
Na kuongeza kuwa "Serikali imesikiliza kilio cha wabunge na katika bajeti ya 2022-2023 imeongeza fedha katika bajeti ya kilimo itakayosaidia kupata mbegu bora na pembejeo pamoja na kuongeza mifereji mipya na kuboresha iliyopo".
Kuhusu swala la wafugaji bajeti Serikali kupitia Wizara ya mifugo inampango kabambe wa kupeleka mbegu bora za ng'ombe wa maziwa pamoja na kuwaelimisha wafugaji kufuga kwa kisasa.
Mwisho.
0 Comments