Header Ads Widget

MADIWANI HALMASHAURI YA MOSHI WAWACHARUKIA WATENDAJI WA VIJIJI.

 


NA WILLIUM PAUL, Moshi.



BARAZA la Madiwani Halmashauri ya wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro limetoa siku thelathini kwa Watendaji wote wa vijiji katika halmashauri hiyo kuhakikisha wanaitisha mikutano ya hadhara na kusoma taarifa za mapato na matumizi.



Kauli hiyo ilitokewa jana na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Moris Makoi katika kikao cha kawaida cha baraza ambapo alisema kuwa, kumekuwa na changamoto kubwa kwa Watendaji kutoitisha mikutano ya hadhara na kusoma taarifa za mapato na matumizi.




Makoi alisema kuwa, baraza hilo linaiagiza ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuanzisha Operesheni ya kuhakikisha kila Mtendaji wa kijiji na kata anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria zilizopo.



"Ni aibu kubwa anafika Waziri katika halmashauri yetu alafu anaenda kwa wananchi anakuta wamefunga ofisi ya Kijiji sababu zake ni kutosomewa mapato na matumizi hili ni aibu na sisi kama baraza hatupo tayari" alisema Makoi.




Mwenyekiti huyo alisema kuwa, ifikapo Juni 30 mwaka huu vijiji vyote viwe vimeshasoma taarifa hiyo ya mapato na matumizi na ziwe zimefika katika kamati ya fedha ili waweze kuzipitia.



Akizingumzia swala la barabara, Mwenyekiti huyo alisema kumekuwa na malalamiko mengi kwenda kwa Wakala wa barabara vijijini (Tarura) kutokana na barabara nyingi kuwa mbovu hivyo wao kama baraza watakutana na Tarura na kufanya ziara ya kutembelea barabara ambazo zimekuwa zikiongoza kwa kulalamikiwa.




"Rais Samia alishasema jukumu la kusimamia barabara zetu ziweze kupitika sio la kuliachia Tarura peke yake hivyo tutapanga na Tarura tufanye ziara ambapo huku tutakutana na Wakandarasi ambao wamekuwa changamoto kubwa ya ucheleweshaji wa miradi kukamilika na sisi tutatoa ushauri wetu ili kuwasaidia Tarura" alisema Makoi.



Katika baraza hilo Madiwani walikataa kupokea taarifa ya utendaji kazi ya Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Moshi (Muwsa) kwa kile walichodai kuwa taarifa hiyo inaupungufu mkubwa huku wakiwaagiza Muwsa kuandaa upya taarifa hiyo.




Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI