Teddy Kilanga _Arusha
Zaidi ya wanafunzi 1200 wamenufaika na programu ya SHE BRAVE yaani kijana shupavu ikiwa ni midahalo ya wanachuo kwa watoto kike kutoka vyuo mbalimbali mkoa wa Arusha katika kukuza usawa wa kijinsia.
Aidha Ili kuhakikisha upatikanaji wa taarifa za ukatili wa kijinsia kwa wahanga wa wanaokabiliwa na changamoto hiyo,Chuo cha Maendeleo ya jamii Tengeru(TICD) wameanzisha mradi wa msaada wa kisheria wenye mrengo wa kumwezesha mtoto wa kike kutambua haki na fursa walizonazo.
Akizungumza Machi 8,2022 katika mdahalo uliowakutanisha baadhi ya wadau wa maendeleo nchini wenye lengo la kukuza masuala mtambuka ya kijinsia na maendeleo ya wanawake nchini, Mratibu wa mradi kituo cha kitaifa cha utafiti na uhifadhi machapisho yahusuyo wanawake (NWRDC) Rose Mtei alisema uanzishwaji wa kituo hicho ni moja ya mikakati ya kuondoa ukatili kwa wanawake.
Mtei alisema kituo hicho kitasaidia wanawake kupaza sauti juu ya upatikanaji wa haki na usawa wa kijinsia pamoja na kuchocheo wajibu wa mwanamke kwenye maeneo ya uchumi,kijamii na kisiasa kitaifa na Kimataifa.
"Kituo hiki kitakuwa kinatoa msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia sambamba na kufuatilia utekelezaji wa sera jinsia pamoja na kuunda mtandao mzuri wa mawasiliano kati ya madirisha ya taarifa za mitandao pamoja na kuunda maktaba ya kidigitali,"alisema Mratibu huyo.
Naye Katibu wa Umoja wa wabunge wanawake wa Jumuiya ya Afrika mashariki (EAC) ambaye ni mbunge kutoka Rwanda, Fatuma Ndagiza alisema EAC imepiga hatua katika kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia kwa kuzingatia kila nchi mwanachama wameanzisha miradi mbalimbali ya kuinua usawa na haki kwa mwanamke.
"Pamoja na uanzishwaji wa miradi hii na msisitizo wa sheria na sera walizojiwekea kila nchi mwanachama wa EAC bado kuna changamoto ukatili wa kijinsia kwa baadhi ya maeneo ikiwemo watoto wakike kuodheshwa wakiwa bado wadogo na masuala la ukeketaji hali inayosababishwa na mila na desturi kandamizi,"alisema.
Mmoja wa wadau hao ambaye pia ni mjumbe wa mtandao wa kijinsia ,Jovita Mlay alisisitiza TICD kujihimarisha kufanya kazi na wizara ya elimu ili kila mwalimu aweze kusoma elimu ya jinsia na pindi atakapokuwa anafundisha wanafunzi awe huru katika ufundishaji wa somo hilo.
Mkurugenzi wa wizara ya maendeleo ya jamii,jinsia,wanawake na makundi maalum,Mwajuma Magwiza alisema Wizara ipo tayari katika kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukuza usawa wa kijinsia katika jamii kwani hali hiyo itasaidia kupambana na vitendo vya ukatili kwa wanawake katika jamii.
0 Comments