Na Bahati Sonda, Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila ameziagiza halmshauri zote za Mkoa wa Simiyu kuhakikisha zinawapa upendeleo wa kuwapa mikopo yenye ukubwa wanawake kutokana na tabia yao njema ya uaminifu wao wa kulipa madeni yao wanayokopa katika 10% zinazotengwa na halmashauri.
Katika mikopo inayotolewa na halmashauri katika makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kundi linaloongoza kulipa madeni ni kundi la wanawake hivyo wanastahili kupewa upendeleo maalum wa kupewa mikopo yenye ukubwa.
Kafulila ameyasema hayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika Kimkoa katika wilaya ya Itilima Mkoani hapa na kusema kuwa ni lazima vikundi vya wanawake vipewe upendeleo huo wa kuongezewa mikopo ktokana na heshima yao ya uaminifu wa kulipa.
Ameeleza kuwa kuongezewa mikopo hakutawafanya kuvunja uaminifu kwa sababu ya kutokulipa madeni kwani wao ni walipaji wazuri badala ya kuwaongezea wale wenye changamoto ya kulipa na kwamba kutokana na uaminifu ni rahisi pia kuaminiwa na Taasisi za fedha.
"Niwaambie wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu kwenye mikopo inayotolewa na halmashauri hakikisheni mnawapa upendeleo maalum wakinamama kwa kuwapa mikopo yenye ukubwa kidogo" Alisema Kafulila
"Ni lazima vikundi vya wanawake vipate mikopo yenye ukubwa kwa sababu tabia yao ni njema pia ni waaminifu na ndiyo maana hata kwenye 10% za mikopo ya halmashauri wanaongoza hivyo kuwaongezea hakutawapa shida" Aliongeza
Katika hatua nyingine amewataka viongozi wanawake wa Mkoa huo wakiwemo wabunge, Madiwani, wakuu wa wilaya, wakurugenzi pamoja na wakuu wa taasisi mbalimbali kukaa kwa pamoja na kupanga namna ya kufanya jambo kwa ajili ya maendeleo ya wanawake na Mkoa huo kwa ujumla huku akisisitiza mshikamano baina yao na kuahidi kushirikiana nao.
Hata hivyo Mkurugenzi wa halmshauri ya wilaya ya Itilima Elizabeth Gumbo akizungumza kwa niaba ya viongozi wanawake wa Mkoa huo alimhakikishia ushirikiano Mkuu wa Mkoa wa Simiyu hususan kwenye suala zima la kusukuma maendeleo.
0 Comments