Serikali imesema kuwa, kwa sasa Tanzania haina mgonjwa hata mmoja aliyebainika kuwa na ugonjwa wa virusi vya polio.
Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na tishio la kuibuka kwa ugonjwa huo katika nchi jirani ya Malawi,ambapo Februari 17 mwaka huu, nchi hiyo ilitangaza rasmi mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya polio.
Hayo yalibainishwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba, wakati akizindua zoezi la chanjo kwa Mkoa huo unaotarajia kuchanja jumla ya watoto 224,455.
Mgumba alisema uwepo wa ugonjwa wa polio katika nchi ya Malawi unaziweka nchi jirani ikiwemo Tanzania katika hali ya hatari ya maambukizi kutokana na muingiliano mkubwa unaosababishwa na shughuli za kiuchumi na biashara.
“Naomba niwatoe hofu wananchi, kwani licha ya kuwepo kwa muingiliano mkubwa kati ya wananchi wa Tanzania na Malawi katika maeneo ya mpakani, lakini hadi sasa hatuna mgonjwa hata mmoja” alisema Mgumba
Alisema mwaka 2015 Shirika la Afya Dunian (WHO) liliitangaza Tanzania kuwa ni miongoni mwa mataifa Duniani yaliyofanikiwa kutokomeza ugonjwa wa virusi vya polio.
Akizungumzia zoezi la chanjo, alisema kwa mujibu wa mapendekezo ya kitaalamu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya nchini kutakuwa na awamu nne za kampeni za kukabiliana na mlipuko wa polio.
Alisema kwa kuanzia kampeni hiyo itahusisha mikoa minne ya Songwe, Mbeya,Njombe na Ruvuma lengo likiwa ni kuwafikia Watoto wote walio chini ya miaka mitano bila kujali hali zao za awali .
Alisema zoezi hilo la chanjo litakuwa ni la siku nne na limeanza jana kuanza kutolewa Machi 24 mwaka huu na kumalizika Machi 27 mwaka huu kwa wataalamu kupita kila nyumba na kutoa chanjo kwa Watoto walio chini ya miaka mitano.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Hamad Nyembea, alisema mkoa huo unatalajia kutoa chanjo ya virusi vya polio kwa Watoto wapatao 224,455.
Dkt Nyembea alitaja chanzo cha ugonjwa wa polio kuwa,huambukizwa kwa njia ya kinywa kwa kula chakula au kunywa maji yenye uambukizo wa kirusi cha polio ambapo humshambulia mtoto na hatimaye husababisha kupooza na kuleta ulemavu wa kudumu.
Naye Mshauri wa kampeni ya polio kutoka UNICEF Alisema baada ya shirika la afya la Dunia wakishirikiana na mashirika mengine ya Afya ikiwemo Unicef wameamua kufanyika kampeni kikanda kuanzia umoja wa nchi za Afrika.
"Tunaanza kampeni ya kikanda Kwa ukanda huu wa nchi za kusini mwa Afrika mbazo ni Tanzania, Zambia, Malawi, Zimbabwe na Msumbiji,uratibu utashirikisha nchi zote za umoja wa nchi za Africa" Alisema mwandamila Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Cosmas Nshenye ambaye pia niMwenyekiti wa wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Songwe, aliahidi kuwa watasimamia zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa ili lilete tija iliyokusudiwa.
0 Comments