Header Ads Widget

MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA XII

 



Adeladius Makwega-DODOMA


Katika matini iliyotangulia, msomaji wangu nilijibu swali moja ambalo liliulizwa na mwanafunzi mmoja wa Tambaza wakati huo ndugu Fredy Mwambene.


Kwa siku ya leo naomba msomaji wangu, kwa hisani yako nikusimulie kisa kimoja juu ya wanafunzi wa Tambaza na hamu yao kuingia Shule ya Sekondari ya Kisutu.


Shule ya Sekondari ya Kisutu ambayo hapo awali ilikuwa ikifahamika kama Dar es Salaam Girs, ilikuwa ni shule ya sekondari nambari mbili kwa ukaribu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyokuwa na ofisi zake Magogoni. Shule ya Sekondari nambari moja jirani ya wizara hii na Ikulu ya Magogoni ilikuwa ni Shule ya Sekondari Forodhani.


Sasa naambiwa shule hii(Forodhani) haipo wamekabidhiwa Wakatoliki. Shule ya msingi jirani na taasisi hizo ilikuwa ni Shule ya Msingi Bunge.


Shule ya Sekondari Kisutu tangu enzi ni shule ya wasichana ambao binafsi nilikuwa navutiwa mno na marinda ya sketi zao aina ya RINDA BOKSI ambayo yalikuwa yakiheshimiana mno na pasi mithili ya tairi la gari moshi na reli.


Wanafunzi wake tangu enzi walikuwa wakivalia sketi za rangi ya damu ya mzee(MAROON) ambayo sasa ni rangi maarufu mno kwa shule za wasichana. Uteuzi wa rangi hii kwa shule za wasichana ulifanywa na walimu makini wa wakati huo kama akina Mama Mramba, Mama Manyahi, Mama Ndosi na walimu wengi akinamama ambao waliwapenda mno wanafunzi wao wa kike.


Shule hii ipo katika eneo ambalo imezungukwa na majengo kadhaa, huku shughuli jirani na hapo ni biashara.


Wanafunzi wa Tambaza mara nyingi walikuwa wakiwahusudu mno wanafunzi wa Kisutu na wakitamani kwenda kuwatembelea lakini kulikuwa na kizingiti kizito.

Tangu enzi Shule ya Sekondari Kisutu ilikuwa na ukuta mkubwa na geti ambalo lilikuwa ngumu kuingia na walinzi makini.


Wanafunzi wa Tambaza jambo hilo liliwauma sana huku wakijiuliza mbona shule ya Jangwani, Zanaki na Forodhani na hata Azania tunaweza kuingia? Kwanini Kisutu ni ngumu?


Jambo hili liliwapa wanafunzi wa Tambaza hamu sana ya kuingia shuleni humo kwa hiyo siku pekee ambayo ilikuwa geti linafunguliwa ni mahafali.


Wakati huo huo hali ya Tambaza ikiwa ya utulivu kwani baada ya mgogoro na mechi ya Tambaza na Jitegemee.


Wanafunzi hao waliamua kushiriki mahafali ya Kisutu wakashuhudie. Jamaa hawa walikutana shuleni Tambaza na kujikusanya huku wengine wakajipiga manukato kidogo kwa kuwa wanaenda shule ya wasichana angalau watokee vizuri.


Jamaa walianza safari kutoka Barabara ya Umoja wa Mataifa kwenda Kisutu mwendo wa kilometa kama tatu hivi kwa miguu huku jamaa mmoja ambaye alikuwa Vespar aliwabeba wenzake watatu na kutanguli katika mahafali hayo.


Mkuu wa Shule ya Kisutu Mama Ndosi alisimama na kumkaribisha mgeni rasmi kutoka wizara ya elimu na kuanza kugawa vyeti vya wahitumu. Wanafunzi wa Tambaza waliotembea kwa miguu walipofika hapo huku majasho yakiwatoka kwanza walienda jikoni kuomba maji ya kunywa kwa wapishi na wakaliona jiko lilipo.


Sasa ndiyo zawadi za wanafunzi waliofanya vizuri zikigawiwa.“Aliyefanya vizuri katika somo la English Language ni...”


Wahitimu wa Kisutu wakiamka huku wakivishana mataji. Vijana wa Tambaza walikaa ukumbini huku wakishuhudia madoido na madaha ya mabinti wa Kisutu katika mahafali hayo.


Katika kundi hilo kuna mwanafunzi mmoja wa Tambaza alikuwa na rafiki yake anayehitimu alimbebea jembe na kumkabidhi huku ukumbini watu wakicheka wa chonjo pengine vijana wa Tambaza wasije kuharibu mahafali haya bure.


Naomba msomaji wangu nikukumbushe kitu, wakati shule ya Tambaza ikiwa na wanafunzi 480 kwa mikondo 12 kwa kidato cha kwanza mwaka 1990, Kisutu walikuwa na wanafunzi 240 kwa mikondo sita tu.


Idadi ya wanafunzi wachache wa kwa Kisutu na hata Forodhani hilo lilisaidia shule hizo za umma kula chakula kizuri sana ambacho wanafunzi wa Tambaza walikuwa wakisema kilikuwa kitamu zaidi ya hata chakula cha nyumbani.


Kumbuka watu wamejaa katika mahafali hayo, harufu ya Pilau iliyokuwa ikitoka jikoni Kisutu iliwashawishi wanafunzi wa Tambaza kunyanyuka ukumbini na kuifuata mithili ya mjusi wa Agamaagama anayemfuata mjusi jike kumpanda.


Wanafunzi wa Tambaza wakafika jikoni hapo ambapo walikufahamu wakati wanaomba maji na kuwakuta wapishi wakitimiza wajibu, hapa pua za wanfunzi hao zilikaribiswa na harufu tamu ya pilau na biriani iliyokuwa ya mgeni rasmi na meza kuu iliyopikwa katika sufuria moja maalumu ambayo ilikuwa ya ujazo kama ya kilogramu 15 hivi.


Wanafunzi mmoja alijitwika sufuri hii ya biriani na kuondoka nayo haraka. Wengine walijitwika majungu mawili ya pilau wakinyanyua kwa pamoja huku wengine wakiruka upande wa pili wa shule hii wa makaburi wakiyapokea majungu hayo mithili ya keki ya harusi ukumbini.


Kule ukumbini waliendelea na mahafali, nao wanafunzi wa Tambaza wakila chakula hicho kando ya makaburi haya, wakianza na biriani ya mgeni rasmi na majungu yale mawili ya pilau.


Chakula hicho kilikuwa kingi mno huku wanafunzi hao wakinunua mifuko ya RAMBO na kuijaza na kuondoka nayo. Wachimba makaburi nao kwa pamoja na kunguru wa eneo la Kisutu wakasherehekea mahafali hayo ya Kisutu kwa mlo huo.


Kilichoendelea ukumbini na mahafali hayo sifahamu. Nina hakika mgeni rasmi hakula biriani ya mahafali hayo.



makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI