Adeladius Makwega-DODOMA
Katika kila siku iendayo kwa Mungu unaposikiliza, unapotazama, kusoma na kufuatilia vyombo vya habari, unaweza kubaini kuwa kuna habari nyingi zinazozihusu Serikali na kuna habari chache za Mahakama.
Bunge, kidogo limejiwekea utaratibu wa miaka mingi wa habari zake kuripotiwa, huku mahakama habari zake anayezitaka, kazi anayo hadi kuzifuata huko walipo. Anayezifuata habari hizo mahakamani, mara nyingi lazima jambo hilo liwe linagusa maslahi yake au ya kundi lake.
Hapo mwanakwetu, wana habari ufunga safari hadi huko mahakamani. Habari zote zinazohusu mahakama huwa juu ya maamuzi ya mahakama, fulani kapelekwa mahakamani! Hakimu fulani kala rushwa! Fulani kapata dhamana!
Lakini nadra mno kusikia mahakama fulani bati zake zimeoza au mazingia yake ni magumu au watendaji wa mahakama hizo hawana hiki na kile. Kama inatokea basi mara moja moja labda mahakama mpya imejengwa au ukarabati umefanyika, hapo zinaoneshwa picha ya mahakama hiyo na sherehe za ufunguzi.
Ngoja niende na mifano.
Dakitari Bingwa anayefanya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili mathalani pale Mloganzila anaweza kutoa huduma yake katika Hospitali ya Mkoa/ Kanda, Hospitali ya Wilaya, katika Kituo cha Afya, na hata katika Zahanati.
‘Nilikuwa safarini nakwenda zangu Songwe, tulipofika njiani, kuna binti alizidiwa ndani ya basi la abiria lililokuwa linatokea Dar es Salaam, akawa anapumua kwa tabu. Dereva alisimamisha basi hilo, huku tukiwa msituni na kondakta aliuliza ndani ya basi kama yupo abiria ambaye ni muuguzi au dakitari. Nilisimama, niliomba abiria wezangu wamshushe nje ya basi hilo binti huyo na walimlaza katika majani na mimi kumsaidia huduma ya kwanza. Mungu bahati binti huyo akapata nafuu na kuanza kupumua vizuri.’
Safari ya basi hilo iliendelea hadi makambako ambapo walipofika tu alipelekwa hosipitali ya wilaya na kulazwa na Dakitari huyo Bingwa kuendelea na safari yake ya Songwe.
Viongozi wa dini wakiwamo Maaskofu na Masheikh wakubwa wamekuwa wakiongoza sala katika makanisa na misikiti ya kawada kabisa wanapotembelea maeneo mbalimbali. Hii ikiwa na maana kubwa sana kwa imani na waamini wa dini hizo.Huku wakitoka makao makuu ya taasisi hizo na kutoa huduma za kiroho katika mazingira ya kawaida kabisa.
Simba na Yanga wawe na mechi ya fainali, ambapo Simba wakishinda wanakuwa mabingwa na Yanga wakishinda wanakuwa mabingwa, akatafutwa refa wa mechi hiyo mwenye beji ya FIFA mfano Maike Dean huyu ni refa mkongwe anayechezesha soka ligi kuu ya Uingereza na UEFA.
Hapo hali itakuwaje?
Hapo mwanakwetu mechi itachezeshwa kwa ueledi mkubwa na pia imani ya wachezaji, viongozi wa timu hizo na mashabiki wa pande zote mbili, huo utakuwa mchezo bora na wa haki.
Hata Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameteua watendaji katika kila kona ya taifa letu kuna wakati huwa anafika hadi katika ngazi ya kitongoji/kijiji akizungumza na wananchi na kutatua kero zao.
Kutokana na mifano hiyo
Kwa muda mrefu nimekuwa najiuliza maswali mawili, hivi kwa nini majaji mara zote wamekuwa wakifanya maamuzi katika Mahakama ya Hakimu Mkaazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa pekee?
Kwanini majaji hao wasiongezewe wigo wao wa kazi na kuingia kufanya maamuzi katika Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya?
Kwa sehemu kubwa Mahakama za Mwanzo ndiyo sehemu kubwa ya Watanzania wanyonge wanapofikisha mashauri yao huko ili yaweze kutatuliwa.
Kitendo cha majaji kubaki kuamua mashauri ya ngazi za juu ya mahakama, hata kama majaji watakuwa waadilifu kiasi gani, bado malalamiko dhidi ya mahakama yatatolewa na kuupa sifa mbaya muhimili huu. Kwani wamekuwa wakitoa huduma hiyo kwa ngazi ya juu mno kuliko ngazi za chini.
Kama Majaji watashiriki kufanya maamuzi mahakama za chini kutakuwa na faida zifuatazo:
Kwanza, maamuzi yao yatatumika kama mfano kwa mahakimu wengi wa mwanzo ambao kwa hakika maamuzi ya mashauri hayo yatakuwa darasa kubwa kwa watendaji wote wa mahakama kwa ngazi za Mahakama iwe za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za hakimu Mkaazi na hata Mahakama Kuu.
Natambua katika hili kuna hoja ya rufaa, kama Jaji kafanya maamuzi ya Mahakama ya Mwanzo alafu hakimu ambaye siyo Jaji anaweza kubatilisha maamuzi hayo kwa ngazi za juu. Hiyo siyo shida, hapo kinachoshindaniwa siyo cheo cha Jaji hapa hoja ni misingi ya kisheria katika maamuzi hayo tu.
Hoja hii italeta ushindani wa misingi ya sheria ndani ya mahakama ambapo sasa upo baina ya Majaji Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani pekee. Ushindani huu unatakiwa kuwagusa na kuwanufaisha watu wa chini pia nayo haki inaweza kupatikana kwa kiwango cha juu zaidi.
Pili, hoja ya maboresho ya Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya katika hali zote yatafanyika kwa kina mathalani namna ya kuhifahi kumbukumbu za mashauri ikiwamo mwenendo wa kesi hizo. Jaji akiwapo siku hiyo basi wasaidizi wa Jaji watasaidia mno makarani, mahakimu na hata wasikilizaji wa kesi namna hukumu inavyotolewa na Jaji akiondoka hali hiyo itaziambukiza mahakama hizi kuwa na hali bora.
Tatu, mahakama kwa baadhi ya watendaji wake wamekuwa wakituhumiwa kwa hoja za rushwa hasa hasa kwa ngazi za chini, kitendo cha Jaji kufika Mahakama ya Mwanzo na kufanya maamuzi ya mashauri hapo kitasaidia mno haki kutendeka mathalani maamuzi ya kesi ya wizi wa mota ya gari, hakuna mtu mwenye uwezo wa kumtafuta jaji kumuhonga chochote katika shauri hilo.
Hapo pande zote mbili zikitambua kuwa Jaji ndiye muamuzi, imani ya haki kupatikana inaingia mawazoni iwe upande wa Jamhuri/Mshitaki au Mshitakiwa.
Nne, kwa waendesha mashitaka, uwepo wa majaji katika kuamua mashauri ya ngazi za chini itasaidia mno kuchapulisha kufanyika kwa uchunguzi wa mashauri hayo na hilo kusaidia kupunguza idadi ya mahabusu katika magereza yetu kwani jambo hilo linagharimi pesa ambazo zingepaswa kwenda kwenye miradi mingine ya maendeleo kama afya na elimu.
Kwa ndugu zetu majaji, hata kama wakashiriki angalau kila juma la mwisho wa mwezi kufika mahakama za mwanzo na kusikiliza mashauri katika mahakama hizo na kutoa hukumu kutakuwa na faida kubwa kwa muhimili huu na taifa letu.
Nayasema haya kwa leo kwa kuwa nina hamu kubwa ya kuwaona Majaji wakihukumu kesi Mahakama za Mwanzo.
Mwanakwetu! Mengine nayaweka kibindoni. Kwa ajili ya siku nyengine.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments