Adeladius Makwega-DODOMA.
Nikiwa kijana mdogo nilikuwa na rafiki yangu mmoja kipenzi niliyekuwa nikisoma naye, akifahamika kama Asha Hamisi Mabarango (Aisha Ngaiza). Baada ya kumaliza shule ya msingi Aisha Hamisi alikwenda kusoma shule ya Sekondari ya Kisutu na mimi kwenda zangu Tambaza.
Mimi nilikuwa namfahamu Aisha vizuri sana na yeye dada yangu huyu alikuwa akinifahamu vizuri sana. Kama ukimpiga Aisha umenipiga mimi na ukinipiga mimi umempiga Aisha.
Aisha alikuwa akijulikana kwetu vizuri sana na mimi nikijulikana kwao vizuri mno. Kwenda mbali zaidi, nilibaini kuwa baba yangu na mama yake Aisha walisoma pamoja shule ya msingi Mbagala wakati huo.
Nilipokuwa nikienda kwao walipokuwa wakiishi kifamilia nilibaini kuwa Aisha alikuwa na bibi yake mzaa mama aliyekuwa akifahamika kama Biti(Binti) Goa na Biti Goa alikuwa na mama yake mzazi aliyekuwa akifahamika kama Biti Pazi.
Hawa mabibi wawili yaani Biti Goa na Biti Pazi ni mtu na mwanawe, kila mmoja alikuwa na tabia zake. Biti Goa alikuwa mkimya mno lakini mama mtu ambaye alikuwa Biti Pazi alikuwa mcheshi sana.
Kwa utamaduni wetu, tulipokuwa tukitoka masomo ya ziada shuleni tulikuwa tunapitia kwa akina Aisha kulipokuwa jirani na shule. Katika safari zangu za kwenda kwa kina Aisha niliwahi kufika nyumbani kwa Biti Pazi na kupata bahati ya kusimuliwa simulizi nyingi mojawapo ni simulizi ni ya kishada.
Alituambia kwamba zamani watoto walikuwa na mchezo uliyokuwa ukifahamika kama KISHADA. Kishada hicho kilikuwa kinatengenezwa na watoto hao kwa pamoja. Kwa hiyo walikuwa wakijipanga vizuri kama kesho watatengeneza kishada walipeana majukumu ya kila mmoja kuja na vifaa vya kutengeneza kishada zikiwamo karatasi, mikasi, nyuzi na vijiti vya kuuunga kishada hicho.
Vifaa vikishakamilika ndipo kazi ya kukata karatasi katika umbo la kishada inafayika na mara nyingi mchezo huo ulichezwa wakati wa jumamosi, jumapili na likizo.
Kishada hicho huwa na umbo kama la mjusi (Guluguja) au samaki kambale. Kazi hiyo kama imemalizika saa za mchana basi hungojea hadi jioni ili kishada kiweze kuruka kwenda mbali zaidi. Kishada hicho ilikuwa ni lazima kiwe na mkia mrefu wa karatasi hapo ndipo huunganishwa na nyuzi ndefu.
Zoezi hilo likikamilika vijana hao huwa tayari kukirusha kishada chao, mara nyingi zoezi hilo hufanyika nyakati za alasiri au jioni kama nilivyokujulisha hapo awali.
Wakati wa kurushwa kishada hicho bingwa wa kuushika uzi vizuri na kutazama muelekeo wa upepo huo husimamia zoezi hilo na wengine wakishangilia kishada kikiwa kinakata mawimbi ya upepo huo angani.
Zoezi hili mara nyingi linafanyika wakati wa hali ya hewa ikiwa imetulia, hakuna mvua kwani kishada mara nyingi kinatengenezwa na karatasi kama kikirushwa msimu wa mvua kishada kitaloa na zoezi hio halitoweza kukamilika.
Kuna wakati uzi unakatika kwa hiyo kishada kitafuatwa kilipoangukia na kufungwa tena na kurushwa hewani kwa mara nyingine.
‘Wakati kishada cha watoto kinarushwa hewani, maranyingi watoto wengine wa upande mwingine wa mtaa huwa wanafanya zoezi hilo hilo na inawezekana wakati wakurusha vishada hivyo vinaweza kukutana huko angani huku vikishindana ni kishada kipi kitakwenda mbali angani zaidi ya kingine.’
Biti Pazi alituuliza je wakati mnatengeneza vishada hivyo sisi tulikuwa tunapewa majukumu gani?
Mmmmm mwanakwetu swali lilikuwa gumu.
Ssote tulikaaa kimya?
Kwani hamjawahi kutengeneza vishada? Biti Pazi alituuliza.
Jibu halikupatikana.
Biti Pazi alimalizia kwa kutuuliza je wewe ni nani wakati wa kutengeza kishada hicho kwa leo? Sote tulikuwa kimya lakini dada yangu Aisha yeye alisema kuwa yeye atakuwa kishada chenyewe kinachotengezwa.
Biti Pazi alicheka sana akasema kuwa sasa wewe kama utakuwa kishada basi wewe utakuwa ni KISHADA MTEMBEZI.
Biti Pazi alimalizia kwa kusema kuwa kama Aisha wewe ni Kishada Mtembezi hakikisha hauruki hovyo hovyo ukavivamia vishada vingine, unapaswa kuruka vizuri wakati wenzako wanakushangilia huku ardhini.
Kweli tuliondoka na sie kurudi majumbani kwetu na kumuacha Biti Pazi nyumbani kwake Mbagala Kwa Mangaya jirani na Mwembe Pacha.
Kweli tangu siku hiyo dada yangu Aisha tulimuita Kishada Mtembezi.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments