Adeladius Makwega-DODOMA
Nikiwa mwanafunzi wa sekondari Ndanda, nikisoma mkoani Mtwara, wakati wa likizo nilikuwa nikisoma masomo ya ziada, angalau nikirudi shuleni nisiwe na tabu kwa kuwa shule nyingi za umma wakati huo zilikuwa na uhaba wa walimu wa kutosha.
Mida ya asubuhi nikiwa katika kituo cha Mbagala Sabasaba ili kuweza kupata usafiri kufika katikati ya Jiji la Dar es Salaam ilikuwa ni wajibu wangu kuvuka Barabara ya Kilwa na kufika kituo cha Basi cha Mpili kilichokuwa jirani na mkahawa maarufu wa wakati huo uliofahamika kama Mpili Tea Room.
Hapa nilipanda basi za Posta au Kivukoni nilitakiwa kugeuza nalo hadi Rangitatu na nilirudi nao hadi Mjini Stesheni, nikienda huko katika masomo ya ziada.
Nikiwa katika Kituo cha Basi cha Mpili, nilikuwa kila siku asubuhi nakutana na watu wawili ambao mara zote walikuwa nadhifu mno na muda mwingine wakivalia tai zao vizuri sana. Jamaa hawa walikuwa warefu kiasi huku wakiwa na wajihi wa rangi nyeusi. Mmoja alikuwa mtu mzima kidogo na mwingine alikuwa kijana.
Kwa kuwa walikuwa watanashati kidogo walikuwa tofauti mno na sie wakaazi wa asili wa Mbagala. Labda utafauti ulikuwa kwa wale walimu na watumishi wengine wa umma. Niliwapenda mno namna jamaa hawa walivyokuwa watanashati.
Baadaye nilibaini kuwa hawa jamaa walikuwa wakifanya kazi na chombo kimoja cha habari kipya wakati huo.
Nakumbuka wakati huo wanahabari hawakuwa wengi, kwa hiyo hata kama mtu anafanya kazi RTD iwe mfanyakazi wa idara yoyote akiwa mtaani kwenu mnamuogopa mno na kumuheshimu sana.
Nakumbuka mtaani kwetu kulikuwa na Dereva wa RTD ambaye alikuwa akifika na gari ya Landrover 110, alifahamika kama Mandwanga tulimuheshimu sana kwani hata maji yakikatika tunamwambia na akienda RTD akiwaambia watangazaji ikisomwa katika Majira tu NUWA kesho yake lazima walete maji mtaani kwetu.
Hawa jamaa wawili niliyokuwa nakutana nao stendi nilimbaini mmoja alikuwa akionekana kusoma habari za michezo na taarifa za habari huko Indepenent Television (ITV) nilimtambua kuwa ni John Ngahyoma.Wakati huo kulikuwa na Runinga ya DTV ambayo ilikuwa na Watangazaji watashati na mahiri kama Pascal Mayala.
Akilini mwangu nilibaki na swali ambalo lilikosa jibu, Je huyu John Ngahyoma ,huyu kijana anayeambatana naye kila asubuhi ni nani?
Kwa kuwa wakati huo muziki wa kizazi kipya ulikuwa unaanza, Msafiri Kondo (Solo Thang)-Ulamaa, Rashidi Hemedi (KBG), Modestus Makwega (Mode Fox), Raymond Mahira (Bunju Mani) na Josephy Mbilinyi (Sugu) MR II walikuwa wakiufanya muziki huo na walikuwa wanakaa Mbagala.
Joseph Mbilinyi alikuwa akiishi Mbagala Mangaya nadhani kwa nduguye mmoja, wakati Msafiri Kondo alikuwa akiishi Mbagala Misheni jirani na makaburi ya Wakristu, jirani pia na Mbagala Spirtual Centre.
Msafiri Kondo yeye alikuwa mwenyeji wa Mbagala, nakumbuka hata dada yake aliyefahamika kama Rehema Mwinyimkuu nilisoma naye shule ya msingi tangu tukiwa watoto, kwa hiyo mimi kwenda kwao na wao kuja kwetu lilikuwa jambo la kawaida sana.
Msafiri Kondo na Joseph Mbilinyi kwa kuwa walikuwa wasanii walifahamiana vizuri, naye Sugu, John Ngahyoma walikuwa wakifahamiana pia. Ndiyo kusema hata yule kijana aliyekuwa anaambatana na John Ngahyoma walimfahamu pia huku wakitokea ukanda mmoja wa asili.
Sugu(Mr II) ambaye baadaye alikuja kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini alimfahamua Solo Thang na kundi lake la Hard Crewz Mob. Kwa kuwa urafiki wa Sugu na vyombo vya habari kama Redio One&ITV ulikuwa karibu na nyimbo zake zikichezwa.
“Yule kijana anafanya kazi Redio one na ITV kama Disc Jockey anaitwa Mike Mhagama na huwa tunampa santuri zetu na anazicheza redioni kwao.”
Waliniambia akina Solo Thang, hapo na mimi nikamfahamu Mike Mhagama ambaye alikuwa DJ na Mtangazaji.
Kwa kuwa utaratibu wa zamani wa RTD ni wa mafundi mitambo walikuwa hawasemi redioni lakini Redio One walikuja na utaratibu mpya kabisa wa redio za kisasa na nyimbo kuchezwa na MADJS.
Kipindi hiki nayo RTD walikuja na redio yao mpya iliyofahamika kama PRT ambayo baadaye ikawa TBC FM ili kuwakamata vijana na nyimbo zao.
Dhana ya muziki huu wa kazazi kipya kuwa ni wa wahuni uliingamiza RTD na ndiyo maana walioshirikiana kwa karibu na wanamuziki hao wa mwanzo unawakuta Redio One na ITV tu.
Kwa hiyo unapotaka kumfahamu zaidi Joseph Haule (Profesa Jay), Mike Mhagama aliyeucheza muziki huo wa kizazi kipya katika hatua za mwanzo anayo mengi ya kusema.
“Sisi wa zamani tulimfahamu kama Nigga Jay, Wakati huo nikiwa DJ wa Redio One, nilikuwa napiga nyimbo nyingi za kizazi kipya kama Bongo Flavour na Bongo Hip hop, mimi sikumfahamu kama mwanamuziki binafsi, bali nilimfahamu kama miongoni mwa wanamuziki wa kundi la Hard Blaterz Mob, yeye Joseph Haule(Nigger Jay), Terry Msiaga-(Fanani Terry), William Shundi-Big Wile (Crazy One).”
Kwa sasa ndugu huyu hayupo Tanzania bali yu Marekani akiyaendesha maisha yake huko.
Je DJ huyu atasema nini zaidi juu ya Joseph Haule?
Subiri matini ijayo.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments