Header Ads Widget

AGRICOM AFRICA NA BENKI YA EQUITY WALETA TABASAMU KWA WAKULIMA

 



Na Fatma Ally MDTV Dar es Salaam


Kampuni ya kilimo ya Agricom Africa leo wametiliana saini mkataba wa makubaliano na Benki ya ya Equity Ili kuruhusu benki hiyo kufadhili vifaa vya kilimo nchini Tanzania kwa lengo la kujenga uwezo na kuongeza tija kwenye Sekta hiyo.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Meneja Uendeshaji wa Kampuni  hiyo, Frank Mushi amesema mkataba huo utawawezesha watu binafsi, wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa, taasisi ndogo za fedha (MFIs) na vyama vya ushirika vinavyojihusisha na kilimo kupata vifaa vya kilimo kuanzia kuandaa shamba mpaka utunzaji maghalani.



Amesema kuwa, katika kubadilisha taswira na tija ya kilimo Tanzania wamezindua kampeni ya Tabasamu Shambani, Tabasamu sokoni Ili kuhakikisha mdau wa kilimo ana uhakika wa vifaa bora na mahitaji ya kifedha katika mnyororo mzima wa thamani kwenye Sekta hiyo, hivyo kufanya kilimo biashara na sio kilimo cha kujikimu kilichogubikwa na unyonge.


Aidha, amesema kuwa, katika makubaliano hayo wamelenga kufanya mambo makubwa manne ikiwemo kukidhi mahitaji ya mkulima wa kisasa kupitia mnyororo mzima wa thamani katika Sekta ya kilimo biashara.


"Utiaji saini wa makubaliano haya kumezindua mpango kabambe wa kutatua changamoto ya ajira kwa vijana ambao ni asilimia 64 ya idadi ya watu wote Tanzania, hivyo kupitia kilimo biashara cha kisasa vijana wengi wataweza kunufaika na huduma ambazo ni rafiki kulingana na mabadiliko ya Teknolojia"amesema Mushi.


Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Alex Duffar amesema makubaliano hayo ni faida kubwa ambapo  kwa sasa wanaendesha kilimo kwa kuangalia mienendo ya ngazi za kimataifa hususani ubora wa vifaa kwa kushirikiana na chapa kubwa zinazoaminika duniani, Teknolojia ya uhifadhi wa kumbukumbu za wateja pamoja na ufuatiliaji wa manunuzi mpaka kukabidhi vifaa.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Tanzania, Isabella Maganga amesema kuwa kutokana na kilimo ndio kipaumbele chao, hivyo wanategemea asilimia 30 ya mikopo wanayotoa itakwenda kwenye kilimo Ili kuweza kuwainua wakulima.



Aidha amesema wanashukuru kuungana na kampuni ya Agricom Africa katika kuhakikisha kila mtu katika mnyororo wa thamani wa kilimo anaweza kupata fedha zinazohitajika kuwezesha uzalishaji bora.


"Dhamira ya Benki ya Equity ni kuhakikisha kuwa jumuiya ya wafanyabiashara wadogo na wakati wanapata suluhisho la kifedha katika hatua zote za mnyororo wa thamani kuanzia uzalishaji mpaka sokoni"amesema Isabella .


Hata hivyo, amesema ni muhimu kwao kuendelea kutoa majukwaa ya kifedha ambayo yatawezesha wafanyabiashara wakubwa wa kilimo wanapata msaada wa kifedha ambao utachangia kuleta mabadiliko ya kilimo, uchumi na maisha mazuri ya watanzania.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI